34

Ndoto hazina maana
1 Mtu mjinga huwa na matumaini ya bure na ya uongo; ndoto humpa mpumbavu mabawa ya kuruka.
2 Kama mtu anayejaribu kushika kivuli na kufukuza upepo ndivyo alivyo mtu anayeamini ndoto.
3 Ndoto ni kama kioo, sura inayoukabili uso.
4 Ni kitu gani kiwezacho kutakaswa na uchafu? Je, ukweli waweza kupatikana kwa uongo?
5 Kupiga bao, ramli na ndoto ni upuuzi; akili huwa na mawazo kama ya mama anayejifungua.
6 Usizitie maanani ndoto isipokuwa kama zimetoka kwa Mungu Mkuu.
7 Maana ndoto zimewadanganya wengi, na wale wanaozitumaini wameaibishwa.
8 Sheria ni kamilifu bila udanganyifu huo, nayo hekima ni kamilifu kwa mtu mwaminifu:

Kusafiri
9 Mtu aliyesafiri sana anajua mengi, na mtu mzoefu wa mengi anajua anachoongea.
10 Mtu ambaye hajakumbana na matatizo hajui mengi, lakini aliyesafiri sana amejipatia maarifa.
11 Katika safari zangu nimeona mengi; ninajua mengi kuliko niwezavyo kuyaeleza.
12 Mara nyingi nimekuwa katika hatari ya kifo, lakini nimechopoka kwa sababu ya maarifa haya.

Kumcha Bwana
13 Wamchao Bwana wataishi, maana tumaini lao liko kwake yeye anayewaokoa.
14 Amchaye Bwana hatakuwa na woga, hawezi kuogopa kwani Bwana ndiye tumaini lake.
15 Heri mtu ambaye anamcha Bwana! Maana anamtazamia yeye amtegemeze.
16 Bwana huwaangalia kwa wema wale wampendao. Yeye ni ngao imara na tegemeo lao thabiti; yeye ni kinga yao mbali na upepo mkali, ni kivuli chao wakati wa jua kali; yeye huwalinda wasijikwae, huwasaidia wasianguke.
17 Bwana huijaza mioyo furaha, na huyatia macho mwanga. Yeye huwapa watu afya, uhai na baraka.

Tambiko
18 Mtu akitoa sadaka kitu kilichopatikana kwa udanganyifu tambiko yake hiyo ina dosari. Zawadi za wasiotii sheria hazikubaliki.
19 Mungu Mkuu hakubali sadaka za wasiomcha, wala wingi wa sadaka hauwezi kuleta upatanisho.
20 Mtu atoaye sadaka kitu alichomnyanganya maskini, ni sawa na mtu anayemuua mtoto mbele ya baba yake.
21 Chakula cha maskini ni uhai wake; yeyote anayempora maskini chakula ni muuaji.
22 Kumnyanganya jirani chakula chake ni kumuua; na kumnyanganya mwajiriwa mshahara wake ni kuua.
23 Mtu mmoja akijenga na mwingine akibomoa, je, wamefanikiwa chochote ila kutoa jasho?
24 Mmoja akimwomba Mungu na mwingine akilaani, je, Bwana ataisikiliza sauti ya nani?
25 Mtu akitawadha baada ya kushika maiti, akaishika tena, je, amepata faida gani kwa kutawadha kwake?
26 Hivyo mtu akifunga kwa ajili ya dhambi zake, kisha akaenda kufanya mambo yaleyale, ni nani atakayesikiliza sala yake? Tena amepata faida gani kwa kujinyenyekesha?

Generic placeholder image