11

1 Ikiwa fukara ni mwenye hekima, anayo sababu ya kujivuna, tena ataketi pamoja na watu mashuhuri. Usiamue kwa sura ya nje
2 Usimsifu mtu kwa sura yake nzuri, wala usimdharau mtu kwa sura yake.
3 Nyuki ni miongoni mwa viumbe vidogo virukavyo, lakini wanachotoa ni kitamu kuliko vitu vyote.
4 Usijivune kwa sababu unavaa nguo maridadi, wala kuvimba kichwa wakati unapopewa heshima. Maana Bwana hufanya mambo ya ajabu, mambo ambayo binadamu hawezi kuelewa.
5 Wafalme wengi wamelazimika kuketi udongoni; na mtu ambaye hakufikiriwa kabisa akavaa taji la kifalme.
6 Watu mashuhuri wengi wameporomoshwa kabisa, wakuu wengi wametiwa makuchani mwa wengine.

Uwe mwangalifu
7 Usimlaumu mtu kabla ya kuchunguza, fikiri kwanza halafu utoe lawama.
8 Sikiliza kabla ya kujibu, wala usimdakize mwingine anapoongea.
9 Usiingilie jambo lisilokuhusu, usijiingize katika ubishi wa wenye dhambi.
10 Mwanangu, usishughulikie mambo mengi mno, ukiongeza shughuli zako hutaepa kulaumiwa. Hata ukijaribu kufuatia sana hutafika, wala hutaweza kutoroka kwa kukimbilia mbali.
11 Watu wengine hufanya kazi kwa bidii sana, lakini mwishowe hujikuta bado wanatindikiwa.
12 Wako na wengine ambao hawana bidii na huhitaji msaada, hawana mali na wamejaa umaskini. Lakini Bwana huwaangalia kwa wema na kuwainua;
13 huwachangamsha na kuwafanya wawe na vitu, hata watu wengine huwaona na kushangaa.
14 Mema na mabaya, uhai na kifo, umaskini na utajiri, vyote hutoka kwa Bwana. [ 15Hekima, elimu na ujuzi wa Sheria hutoka kwa Bwana; upendo na kujua kutenda mema hutoka kwake; 16uhalifu na giza viliumbwa kwa ajili ya wenye dhambi; wanaopenda ubaya watazeeka katika ubaya.]
17 Zawadi za Bwana ni hakika kwa wenye kumcha, wema wake utakuwako daima kuwaongoza.
18 Watu wengine huwa matajiri kwa bidii na nguvu, lakini tuzo wanalopata ni hili:
19 Ingawa wanasema: “Sasa naweza kustarehe, na kufurahia faida niliyopata,” hawajui itadumu muda gani; watakufa na kuwaachia wengine utajiri wao.
20 Wewe shikilia wajibu wako, zeeka ukiwa kazini mwako.
21 Usistaajabie kazi za wenye dhambi, lakini mtumaini Bwana na fanya kazi yako. Maana kwa Bwana ni jambo rahisi sana kumtajirisha maskini mara moja.
22 Wema watapokea baraka ya Mungu. Mungu huwabariki mara moja.
23 Usiseme, “Ninahitaji nini zaidi? Nitapata nini wakati ujao?”
24 Tena, usiseme, “Nina kila kitu cha kunitosheleza. Ni maafa gani yatakayoweza kunipata?”
25 Wakati wa fanaka mtu husahau matatizo; na wakati wa matatizo hakuna akumbukaye fanaka.
26 Maana, kwa Bwana ni jambo rahisi mtu anapokufa, kumtuza kadiri ya matendo yake.
27 Matatizo ya muda mfupi tu humsahaulisha mtu raha; mtu hujulikana alivyo mwishoni mwa uhai wake.
28 Usiseme fulani ana heri kabla hajafa, maana ushahidi wote hutolewa baada ya kufa.

Uwe mwangalifu kuchagua marafiki
29 Usikaribishe kila mtu nyumbani kwako; maana mitego ya wajanja ni mingi.
30 Mtu mwenye majivuno ni kama chombo cha kukutia hatarini, kama jasusi, atachunguza udhaifu wako.
31 Atageuza mambo mema yaonekane kuwa maovu, na kuona kosa katika matendo mema kabisa.
32 Cheche moja huwasha rundo la makaa, na mwenye dhambi huvizia kumwaga damu.
33 Jihadhari na mfidhuli na matendo yake ya ulaghai, la sivyo atakuletea dosari ya kudumu.
34 Mkaribishe nyumbani mtu mgeni naye atazusha mzozo; atakufanya ufarakane na jamaa yako mwenyewe.

Generic placeholder image