8

Kutumia akili
1 Usishindane na mtu mwenye uwezo, la sivyo utajikuta makuchani mwake.
2 Usigombane na mtu yeyote tajiri, la sivyo utajiri wake utakushinda mahakamani. Maana dhahabu imewaangamiza wengi na kuipotosha mioyo ya wafalme.
3 Usibishane na mtu anayepayukapayuka; usiongeze kuni katika moto wake.
4 Usitaniane na mtu asiye na adabu, la sivyo atawafedhehesha wazee wako.
5 Usimdharau mtu aliyetubu dhambi. Kumbuka sote tuna hatia.
6 Usimbeze mtu yeyote aliye mzee, maana baadhi yetu tunakuwa wazee.
7 Usifurahie kifo cha mtu yeyote. Kumbuka sisi sote lazima tufe.
8 Usidharau misemo ya wenye hekima bali jitahidi kufahamu mafumbo yao; maana kutokana na hayo utajifunza mbinu na mtindo wa kuwatumikia wakuu.
9 Usipuuze wanayosema wazee, maana wao pia walifunzwa na baba zao. Utajifunza kutoka kwao namna ya kufikiri na ufundi wa kutoa jibu wakati wake.
10 Usichochee moto wa mwenye dhambi; usije ukajichubua nawe kwa moto wake.
11 Usikubali kuongozwa na fidhuli, asije akajaribu kukunasa kwa maneno yako.
12 Usimkopeshe mtu mwenye nguvu kuliko wewe; kama ukimkopesha kitu, ujue kuwa kimepotea.
13 Usitoe dhamana kuliko uwezo wako, ukiwa mdhamini, basi uwe tayari kulipa.
14 Usimshtaki hakimu mahakamani, maana hukumu itatolewa kwa kumpendelea yeye.
15 Usisafiri pamoja na mtu mzembe, asije akawa mzigo kwako; maana atatenda aongozwavyo na hisi zake, nanyi wawili mtaangamia kwa ujinga wake.
16 Usibishane na mtu akasirikaye haraka, wala usisafiri naye mahali kusiko na watu; maana kwake kumwaga damu si kitu, na huko kusiko na msaada, atakushambulia.
17 Usiombe ushauri kwa mtu mpumbavu, maana yeye hataweza kutunza siri.
18 Usifanye lolote la siri mbele ya mgeni, maana hujui atafanya nini na siri hiyo.
19 Usimfungulie kila mtu yaliyo moyoni mwako, wala usikubali yeyote akupendelee.

Generic placeholder image