31

Fedha huleta matatizo
1 Kukosa usingizi juu ya mali humdhoofisha mtu; kuhangaika juu yake huondoa usingizi.
2 Mahangaiko ya usiku kucha hufukuza usingizi, ni kama ugonjwa mkali, huondoa kabisa usingizi.
3 Tajiri hutoa jasho na kuchuma mali nyingi, kisha huketi chini na kuponda maisha.
4 Maskini naye hutoa jasho na mali yake hupungua, kisha huketi chini na hana chochote.
5 Apendaye dhahabu hataonekana bila hatia, na atafutaye sana fedha atapotoshwa nayo.
6 Wengi wameangamia kwa sababu ya mali, na maangamizi hayo yamewavamia ana kwa ana.
7 Mali ni mtego kwa wanaovutwa nazo, na kila mpumbavu atanaswa nazo.
8 Heri mtu aliye tajiri bila kuwa na lawama, mtu ambaye hakimbilii utajiri.
9 Ni nani huyo, tumpe hongera? Maana amefanya maajabu kati ya watu.
10 Nani aliyepata kujaribiwa na mali akaonekana bila hatia? Mtu kama huyo anayo haki kujivuna! Nani aliyepata nafasi ya kutenda dhambi asitende? Nani aliyepata nafasi ya kufanya maovu asifanye?
11 Mtu kama huyo mali yake itadumu, na jumuiya itautambua ukarimu wake.

Karamu
12 Ukikaribishwa kwenye karamu kubwa, usiwe na uchu mkubwa wa chakula wala usiseme, “Kuna chakula kingi kweli!”
13 Kumbuka kuwa jicho la ulafi ni kitu kibaya. Je, kuna kitu chenye ulafi kama jicho? Ndiyo maana jicho hutoa machozi daima.
14 Usinyoshe mkono kuchukua anachotaka mwingine, wala usimpige kumbo mwenzako kujipatia chakula.
15 Tambua hali ya mwenzako unavyofikiria wewe mwenyewe, na uwajali wengine kwa kila njia.
16 Kula unachopewa kama mtu mwenye adabu, wala usitafune harakaharaka la sivyo utachukiwa.
17 Ni tabia njema kuwa wa kwanza kuacha kula, usiwe mlafi usije ukawaudhi watu.
18 Kama umeketi pamoja na watu wangu, usiwe wa kwanza kuchukua chakula.
19 Chakula kidogo ni kingi kwa mwenye adabu, na hatahangaika akirudi nyumbani kwake.
20 Mtu alaye kiasi hupata usingizi mzuri, ataamka mapema na kujisikia mchangamfu. Lakini mlafi atakosa usingizi, atajisikia kichefuchefu na msokoto wa tumbo.
21 Ikiwa umelazimika kula mno ondoka ukatapike nawe utapata nafuu.
22 Nisikilize mwanangu, wala usinipuuze, na mwishowe utatambua niliyosema. Uwe na bidii katika kazi zako zote, nawe hutapatwa na ugonjwa wowote.
23 Watu humsifu aliyemkarimu kwa chakula, na maoni yao juu ya wema wake ni kweli.
24 Mchoyo wa chakula atasemwa kijijini kote, na maoni yao juu ya uchoyo wake ni kweli.

Pombe iliumbwa kumfurahisha mtu
25 Usijioneshe kuwa hodari wa kunywa pombe, maana pombe imewaangamiza wengi.
26 Tanuri hupima ugumu wa chuma, na pombe hupima mioyo katika shindano la wenye kiburi.
27 Pombe ni kama uhai kwa mtu ukinywa kwa kiasi. Maisha yafaa nini bila pombe? Imeumbwa iwafurahishe watu.
28 Kunywa pombe wakati wake na kwa kiasi, kwaleta shangwe moyoni na furaha rohoni.
29 Lakini kunywa pombe kupita kiasi, kunaleta kuumwa kichwa, uchungu na fedheha.
30 Ulevi huongeza hasira ya mpumbavu akajiumiza mwenyewe; humdhoofisha na kumwongezea majeraha.
31 Usimkaripie jirani yako kwenye pombe, wala usimdharau anapofurahia karamu. Usimwambie neno la kumwonya, wala usimsumbue kwa kumtaka alipe deni.

Generic placeholder image