40

Unyonge wa binadamu
1 Majukumu magumu yaliumbwa kwa ajili ya binadamu wote, mzigo mzito uko juu ya wanaadamu tangu walipozaliwa mpaka watakaporudi kwao mavumbini, ambayo ni mama wa watu wote.
2 Wasiwasi wao, hofu ya moyoni, na woga wao ni juu ya siku ya kufa.
3 Hayo huwapata wote: Tangu mfalme katika fahari yake, mpaka mnyonge anayeketi mavumbini na katika majivu;
4 tangu tajiri na mavazi yake ya zambarau na taji kichwani, mpaka yule maskini avaaye magunia.
5 Kila kitu ni hasira na wivu, shida na wasiwasi, hofu ya kifo, uadui na ugomvi. Hata mtu anapolala kitandani mwake usingizi wake huvuruga mawazo yake.
6 Hulala usingizi kidogo au halali kabisa; na akiwa amelala, huwa kama yu macho. Husumbuliwa na maono akilini mwake, kama mtu aliyetoroka mstari wa mbele vitani.
7 Wakati wa kuokolewa, huamka, akashangaa kwamba hofu zake hazikuwa kweli.
8 Ndivyo ilivyo kwa viumbe wote, binadamu na wanyama, na kwa wenye dhambi ni mara saba:
9 Kila mara kifo, umwagaji damu, mapigano na vita, maafa, njaa, mateso na tauni.
10 Hayo yote yaliumbwa kwa ajili ya wenye dhambi, na kwa sababu ya waovu gharika ilikuja.
11 Vitu vyote vilivyotoka ardhini vitarudi ardhini, kama vile maji yote hurudi baharini.

Misemo mbalimbali
12 Kila rushwa na udhalimu, vitafutwa, lakini imani njema itadumu milele.
13 Mali ya waovu itakauka kama kijito, itapondeka kwa kishindo kama ngurumo wakati wa mvua nyingi.
14 Mtu mkarimu atapata furaha, lakini wakosefu wataangamia kabisa.
15 Watoto wa wasiomcha Mungu hawatakuwa na chipukizi, wao ni kama mizizi dhaifu kwenye mwamba mtupu.
16 Matete yaliyo kando ya maji au mto, hayo ndiyo yatakayongolewa kabla ya nyasi nyingine.
17 Wema ni kama bustani iliyojaa baraka, na sadaka kwa maskini hudumu milele.

Furaha za maisha ya binadamu
18 Kwa anayejitegemea na mfanyakazi maisha ni mazuri; lakini bora kuliko hiyo ni mtu anayegundua hazina.
19 Kuwa na watoto na kujenga mji humpatia mtu jina, lakini mke asiye na hatia ni bora kuliko hivyo viwili.
20 Pombe na muziki hufurahisha moyo, lakini kuipenda hekima ni bora kuliko hivyo viwili.
21 Filimbi na kinanda hutoa muziki mtamu, lakini sauti ya kupendeza ni bora zaidi.
22 Macho hufurahia urembo na uzuri wa mtu, lakini uzuri wa chipukizi za mbegu ni bora zaidi.
23 Rafiki na ndugu hufaa sana, lakini kupatana kwa mke na mumewe ni bora zaidi.
24 Kuwa na ndugu na msaada wakati wa shida ni vizuri, lakini kuwasaidia maskini huokoa kuliko hivyo.
25 Dhahabu na fedha humfanya mtu imara, lakini shauri jema lathaminiwa kuliko hivyo viwili.
26 Mali na nguvu humfanya mtu kuwa thabiti, lakini kumcha Bwana ni bora zaidi. Hakuna dosari katika kumcha Bwana, na ukiwa na kipaji hicho huhitaji msaada.
27 Kumcha Bwana ni kama bustani ya baraka, nayo humlinda mtu kuliko fahari yoyote.

Kuombaomba
28 Mwanangu usiishi maisha ya kuombaomba, ni afadhali kufa kuliko kuombaomba.
29 Mtu anapomtegemea mwingine ampe chakula, anaishi maisha ambayo hayastahili utu. Kutegemea chakula cha mwingine ni kujiaibisha; mtu mwenye akili, aliyefunzwa vema ataepa kuishi hivyo.
30 Kwa mtu asiye na aibu kuombaomba ni kutamu, lakini ndani yake kuna moto unaomchoma.

Generic placeholder image