19

1 Mfanyakazi mlevi hatakuwa tajiri. Anayepuuza mambo madogo ataanguka kidogokidogo.
2 Pombe na wanawake huwapotosha wanaume wenye akili; mwanamume afanyaye urafiki na malaya ni mpotovu kabisa.
3 Huyo mwisho wake ni kuoza na kuliwa na wadudu; maisha yake ya uzembe yataondolewa.
4 Anayewatumainia wengine haraka mno, hana akili. Na atendaye dhambi, anajidhuru mwenyewe.
5 Anayefurahia uovu, atahukumiwa.

Kupiga domo kaya
6 Anayechukia domo kaya, anajiepusha na uovu.
7 Usirudie kitu ulichoambiwa, nawe hutapata madhara yoyote.
8 Usimwambie mtu awe rafiki au adui, isipokuwa tu kama ni dhambi kwako kunyamaza.
9 Maana huenda fulani alikusikia na kukuona, na wakati ukitimia, atakuchukia.
10 Je, umewahi kusikia kitu? Na kife pamoja nawe. Lakini usiogope! Hilo halitakupasua!
11 Mpumbavu anayejaribu kuficha neno lolote, atasikia machungu kama mama anayejifungua.
12 Kama vile mshale uliompenya mtu pajani ndivyo ilivyo neno ndani yake mpumbavu.
13 Ukisikia rafiki amefanya kosa, mwulize. Huenda si kweli; na kama ni kweli, hatarudia.
14 Mwulize jirani; labda hakusema. Na kama alisema, hatasema tena.
15 Mwulize rafiki uliyoyasikia, labda hakuyasema. Kwa hiyo usiamini kila kitu unachosikia.
16 Maana mtu aweza akakosea bila kukusudia. Nani ambaye hajawahi kukosa kwa ulimi wake?
17 Ukisikia kitu juu ya jirani; mwulize, usimtishe! Ipe nafasi sheria ya Mungu Mkuu ifanye kazi. [Na usiwe na hasira. 18Kumcha Bwana ni mwanzo wa kukubaliwa naye, na kuwa na hekima kunakufanya akupende. 19Kuzijua amri za Bwana kunaleta maisha yenye nidhamu; na wale wanaompendeza watafurahia matunda ya mti wa uzima.]

Hekima ya kweli
20 Hekima yote ni kumcha Bwana;
21 na hekima yote yahusu kutii sheria. [Kujua Bwana ni mwenye enzi kuu. Mtumishi anapomwambia Bwana wake, “Sitafanya unalotaka,” hata kama atafanya baadaye, anamkasirisha huyo bwana anayemtegemeza.]
22 Lakini kujua uovu si hekima, mashauri ya wenye dhambi sio busara.
23 Uko ujanja ambao ni chukizo tupu. Lakini yuko mpumbavu ambaye hana tu hekima.
24 Afadhali mtu mcha Mungu asiye na akili kuliko mtu mwerevu sana ambaye anavunja sheria.
25 Kuna walio wajanja sana na hawatendi mambo ya haki; wako na wengine wanaopotosha wema kupata haki zake.
26 Wako watu walaghai wanaojidai wana huzuni, lakini ndani wamejaa udanganyifu mtupu.
27 Hao huficha nyuso zao na kujidai hawasikii; lakini kama hawaonekani watakuangamiza.
28 Na kama hawana nguvu ya kutenda dhambi, watakapopata nafasi, wataitenda tu.
29 Mtu hujulikana kwa namna anavyoonekana, na mwenye busara utamtambua ukikutana naye.
30 Mtu alivyovaa, anavyocheka na kutembea, vyote vinamwonesha jinsi alivyo.

Generic placeholder image