48

Elia
1 Kisha alizuka nabii Elia kama moto; na maneno yake yaliwaka kama mwenge.
2 Aliwaletea watu njaa, na kwa bidii yake ya kumpenda Mungu akawafanya wawe wachache.
3 Kwa neno la Bwana alizifunga mbingu, na mara tatu akaleta moto.
4 Kweli ewe Elia ulitukuka sana kwa matendo yako ya ajabu! Hakuna mtu anayestahili kujivuna kama wewe?
5 Wewe ulimfufua maiti; kwa neno la Mungu Mkuu ukamwondoa ahera.
6 Uliwaporomosha wafalme na kuwaangamiza; na watu maarufu ukawafanya wawe wagonjwa.
7 Wewe ulisikia makaripio huko Sinai, na tangazo la adhabu huko Horebu.
8 Ulimpaka mafuta mfalme awaadhibu watu, na manabii wa kushika mahali pako.
9 Ulichukuliwa mbinguni kwa kimbunga cha moto, katika gari la farasi wa moto.
10 Imeandikwa kuwa ulikuwa tayari kila wakati wake, kuituliza ghadhabu ya Mungu kabla haijalipuka kwa wingi, ukamfanya baba na mtoto kupatana, na kuyarekebisha makabila ya Yakobo.
11 Heri wale waliokuona wakafariki; lakini heri yako wewe zaidi maana waishi.

Elisha
12 Elia alipotoweka katika kimbunga Elisha alijazwa nguvu za Elia. Maisha yake yote hakutetemeka mbele ya mfalme, wala hakuna mtu yeyote aliyekuwa na uwezo juu yake.
13 Hakuna jambo lililokuwa gumu kwake, na alipokwisha kufa mwili wake ulitoa unabii.
14 Kama alivyotenda maajabu akiwa hai, hata alipokwisha kufa alitenda maajabu.
15 Hata kwa hayo yote watu hawakutubu. Hawakuziacha dhambi zao, mpaka wakachukuliwa mateka mbali na makwao, wakatawanywa duniani kote. Watu waliobaki nchini walikuwa wachache sana, walitawaliwa na wazawa wa Daudi.
16 Baadhi yao walimpendeza Bwana, lakini wengine walizidi kutenda dhambi.

Hezekia
17 Hezekia aliujengea ngome mji wake, na kuleta maji ndani kwa mfereji. Alichimba mtaro kwa chuma kwenye mwamba mgumu, na kujenga mabawa ya maji.
18 Katika siku zake Senakeribu alimshambulia, akamtuma mkuu wa vikosi vyake, akaushambulia mji wa Siyoni, na kujigamba sana kwa kiburi.
19 Kisha mioyo ya Waisraeli ikadunda na mikono ikatetemeka, wakawa katika taabu kama mwanamke anayejifungua.
20 Lakini walimwita Bwana mwenye huruma, wakimwinulia mikono yao. Naye Mtakatifu akawasikia mara kutoka mbinguni, akawakomboa kwa mkono wa Isaya.
21 Bwana akaipiga kambi ya Waashuru, na malaika wake akawafutilia mbali.
22 Hezekia alitenda mema akazingatia nyayo za Daudi, babu yake, kama alivyoamuru nabii Isaya ambaye aliaminika kabisa katika maono yake.
23 Nyakati zake Isaya jua lilirudi nyuma, akayarefusha maisha ya mfalme.
24 Kwa nguvu za roho aliyaona mambo ya mwisho, akawafariji waliokuwa wanaomboleza mjini Siyoni.
25 Aliwafunulia mambo yatakayotukia mwishoni, akawaambia mambo ya siri kabla ya kutukia kwake.

Generic placeholder image