14

1 Heri mtu asiyekosea kwa ulimi wake; hahitaji kusikitika kuwa amekosa.
2 Heri mtu ambaye dhamiri yake haimshtaki, na ambaye hajakata tamaa.

Matumizi ya mali
3 Si sawa kwa mtu mchoyo kuwa tajiri. Utajiri una maana gani kwa mtu bahili?
4 Mtu anayekusanya mali kwa kujinyima mwenyewe, anawakusanyia watu wengine. Hao wataiponda mali yake katika anasa.
5 Aliye bahili kwake mwenyewe atakuwa mkarimu kwa nani, kama hafurahii utajiri wake mwenyewe?
6 Hakuna mtu bahili kuliko anayejichukia mwenyewe; ndivyo ubaya wake unavyomlipa yeye mwenyewe.
7 Hata kama akitenda wema, hutenda kwa ajali, na mwishowe hujulisha hali yake duni.
8 Mtu mwenye kijicho ni mwovu; huangalia pembeni na kuwadharau watu.
9 Jicho la mchoyo haliridhiki na kile alicho nacho, na uchoyo huidhoofisha roho.
10 Mtu mchoyo ni bahili wa chakula, haweki chakula mezani pake.
11 Mwanangu, tumia vitu vyako kukufurahisha uwezavyo, na mtolee Bwana tambiko zitakiwazo.
12 Kumbuka kwamba kifo hakitakawia, na kwamba hujatangaziwa kauli ya kuzimu.
13 Mtendee rafiki yako mema kabla hujafa; uwe mkarimu na kumpa kadiri ya uwezo wako.
14 Usijinyime siku moja ya furaha, usiache sehemu yako ya furaha halali ikuponyoke.
15 Siku moja utawaachia wengine matunda ya jasho lako; yote uliyochuma kwa kazi ngumu yatagawanywa kwa kura.
16 Wape wengine na kupokea kwao ujifurahishe moyo, maana mtu hatazamii starehe huko kuzimu.
17 Viumbe vyote hai huchakaa kama vazi, maana kauli ya tangu zama ni: “Lazima mtakufa!”
18 Kama vile majani katika mti uliotanda matawi: Hupukutika yakaanguka na mengine huota, ndivyo ilivyo kwa binadamu wenye mwili na damu: Mmoja hufa na mwingine huzaliwa.
19 Kila kilichotengenezwa huchakaa na kutoweka, naye mtengenezaji hutoweka na kazi yake.

Furaha ya kuwa na Hekima
20 Heri mtu anayetafakari juu ya Hekima mtu anayefikiri kwa busara.
21 Yule anayezifikiria njia za Hekima, na kuwaza na kuwazua pia juu ya siri zake.
22 Mtu amtafutaye Hekima kama vile mwindaji, na kukaa kwenye njia zake kumngojea.
23 Mwenye kuchungulia madirishani mwake, na kusikiliza milangoni mwake.
24 Mwenye makazi yake karibu na nyumba yake na kufunga kigingi cha hema lake ukutani mwake.
25 Mwenye kusimika hema lake karibu naye na kukaa katika makao yake mazuri.
26 Huweka watoto wake chini ya ulinzi wake, na kupumzika chini ya matawi yake.
27 Kwake atapata kivuli cha kumkinga na joto, na kukaa katika fahari yake.

Generic placeholder image