23

1 Ee Bwana, Baba na Mtawala wa maisha yangu, usiniache niangamizwe na maneno yangu, wala usikubali nifanye makosa kwa sababu yake!
2 Laiti mawazo yangu yangechapwa fimbo, na moyo wangu ungefunzwa nidhamu ya busara. Hapo singeachwa kukosolewa makosa yangu, na dhambi yangu yoyote kuadhibiwa;
3 ili makosa yangu yasiongezeke zaidi, na dhambi zangu zisiwe nyingi. Hapo sitaanguka mikononi mwa maadui zangu; maadui zangu hawatafurahi dhidi yangu.
4 Ee Bwana, Baba na Mtawala wa maisha yangu, nakuomba nisiwe na majivuno.
5 Nakuomba uniondolee tamaa mbaya.
6 Usiruhusu niwe mchoyo au niwe na tamaa mbaya. Usiniache kutawaliwa na tamaa hizo mbaya.

Kuapa
7 Wanangu, sikilizeni mafunzo kuhusu kusema vizuri; mtu atakayefuata hayo hatanaswa mitegoni.
8 Mwenye dhambi hukamatwa kwa maneno yake, wafidhuli na wenye kiburi hunaswa nayo.
9 Usiuzoeshe mdomo wako kuapa, wala kuzoea kutaja jina la Mungu Mtakatifu.
10 Maana kama mtumishi anayechunguliwa sana, naye hatakosa kuchapwa viboko, vivyo hivyo anayeapa daima kwa kutaja jina la Mungu, hakika hataepukana na dhambi.
11 Mtu anayeapa kwa wingi amejaa uovu, na majanga hayatatoka nyumbani kwake. Akikiuka kiapo chake atakuwa na hatia; na akikidharau atakuwa na hatia maradufu. Kama ameapa bure hatafikiriwa kuwa hana kosa, hata hivyo ni mkosaji tu, ataadhibiwa; na nyumbani kwake kutakuwa na maafa daima.

Mazungumzo machafu
12 Kuna namna ya kusema ambayo ni kama kifo. Hiyo na isiwepo kamwe katika wazawa wa Yakobo. Wamchao Mungu watayaepa makosa hayo yote hawatagaagaa katika dhambi.
13 Usiuzoeshe mdomo wako kusema machafu, maana kusema hivyo kunahusika na dhambi.
14 Unapoketi miongoni mwa wakuu kumbuka baba yako na mama yako, usije ukawasahau mbele ya hao wakuu, ukaonekana kuwa mpumbavu kwa tabia yako. Hapo utatamani kuwa heri usingelizaliwa na kuilaani siku ile ulipozaliwa.
15 Mtu aliyezoea kutumia lugha chafu kamwe hatakuwa na nidhamu maishani.

Zinaa
16 Watu wa namna mbili hurudiarudia dhambi, na namna ya tatu husababisha ghadhabu ya Mungu. Mtu anawaka tamaa kama moto na hawezi kupoa mpaka imezimwa. Mtu anakuwa na tamaa kuzini na mwili wake mwenyewe na hataacha mpaka yeye mwenyewe ameteketezwa.
17 Kwa mzinzi, kila cha kula ni kitamu, hatachoka nacho mpaka amekufa!
18 Mtu anavunja nadhiri yake ya ndoa na kujisemea: “Nani ananiona? Giza limenizunguka na ukuta umenificha! Hakuna mtu anayeniona, ya nini niogope? Mungu Mkuu hataona dhambi yangu!”
19 Woga wa mtu huyo ni kwa watu tu. Hajui kuwa macho ya Bwana ni maangavu mara elfu kumi kuliko jua. Yanaziona njia zote za binadamu, hata zile sehemu zote zilizofichika.
20 Kabla ulimwengu haujaumbwa, ulijulikana kwake; hata baada ya ulimwengu kumalizika kuumbwa.
21 Mtu huyo ataadhibiwa mji wote ukitazama, atakamatwa wakati ambapo hatazamii kabisa.
22 Ndivyo ilivyo pia kwa mwanamke anayemwacha mumewe, akazaa watoto na mwanamume mwingine.
23 Kwanza, mwanamke huyo amekaidi sheria ya Mungu Mkuu; pili, amefanya kosa dhidi ya mumewe; na tatu, amefanya uzinzi kwa umalaya wake, akazaa watoto kwa mwanamume mwingine.
24 Yeye mwenyewe ataletwa mbele ya baraza, na atakabiliwa na adhabu kuhusu watoto wake.
25 Watoto wake hawatadumu imara, chipukizi hao wake hawatakuwa na matunda.
26 Ataacha duniani kumbukumbu la laana; aibu aliyoifanya haitafutwa kamwe.
27 Wale watakaoachwa hai baada yake watatambua kuwa hakuna lililo bora kuliko kumcha Bwana, na hakuna kilicho kitamu kuliko kutii amri za Bwana.

Generic placeholder image