2

Uaminifu kwa Mungu
1 Mwanangu, ukienda kumtumikia Bwana, uwe tayari kupata majaribu.
2 Uwe mnyofu wa moyo na nia moja; na usihangaike wakati wa taabu.
3 Ambatana na Bwana wala usimwache kamwe, nawe utafanikiwa mwishoni mwa maisha yako.
4 Uyapokee yote yatakayokupata, hata ukiaibishwa uwe na uvumilivu,
5 maana dhahabu hujaribiwa kwa moto na watu wanaokubaliwa na Mungu kwa tanuri ya aibu.
6 Mtegemee Mungu, naye atakusaidia, shika njia nyofu na kumtumaini yeye.
7 Enyi mnaomcha Bwana ngojeni huruma yake, msigeuke upande, msije mkaanguka.
8 Enyi mnaomcha Bwana, mtumainini yeye, nanyi hamtakosa tuzo lenu.
9 Enyi mnaomcha Bwana muwe na tumaini la fanaka; mtazamie kupata furaha ya milele na huruma.
10 Fikirini juu ya vizazi vilivyopita mkajiulize: “Nani aliyepata kumtegemea Bwana, akaaibika? Nani aliyedumu katika kumcha Bwana, akaachwa naye? Nani aliyemwomba Bwana, akasahauliwa naye?
11 Maana Bwana ni mpole na mwenye huruma. Yeye husamehe watu dhambi na kuokoa wakati wa shida.
12 “Ole wake mtu asiye imara moyoni na anayelegalega! Ole wake mwenye dhambi anayefuata njia mbili!
13 Ole wake mtu aliye mwoga moyoni asiye na tumaini! Mtu wa namna hiyo hatalindwa.
14 Ole wenu nyinyi mliopoteza matumaini yenu; mtafanya nini Mungu atakapofika kuwaadhibu?
15 Wanaomcha Bwana hawaachi kamwe kutii maneno yake; wale wanaompenda huzifuata njia zake.
16 Wanaomcha Bwana hutafuta kumpendeza, wale wanaompenda huzingatia sheria yake.
17 Wanaomcha Bwana wako tayari daima kumtumikia, Wao hunyenyekea mbele yake na kusema:
18 Tujiweke mikononi mwa Bwana na sio mikononi mwa watu ambao hufa. Maana kama ulivyo ukuu wake ndivyo pia huruma yake.”

Generic placeholder image