18

Ukuu wa Mungu
1 Yeye aishiye milele aliumba ulimwengu wote.
2 Bwana peke yake ndiye atendaye kwa uadilifu. [Na hakuna mwingine isipokuwa yeye. 3Huuongoza ulimwengu kwa kiganja cha mkono wake, na kila kitu hutii matakwa yake. Yeye ni mfalme wa vitu vyote, na nguvu zake hutenganisha kati ya kilicho kitakatifu na kilicho najisi.]
4 Hajampa yeyote uwezo wa kutosha kutangaza kazi zake, na wala hakuna mtu awezaye kuzichunguza.
5 Nani anaweza kupima nguvu zake kuu? Nani anaweza kuhesabu kikamilifu rehema zake?
6 Haiwezekani kuzipunguza au kuziongeza. Haiwezekani kuyaelewa maajabu ya Bwana.
7 Binadamu anapofikia mwisho wa hayo anajikuta kwamba ndio tu anaanza; na akiacha, anabaki katika bumbuazi.

Mtu si kitu
8 Mtu ni nini na anafaa nini? Uzuri wake ni nini na ubaya wake ni nini?
9 Mtu akiishi miaka 100, ameishi maisha marefu.
10 Lakini kama vile tone la maji kutoka baharini, na kama chembe ya mchanga wa pwani, ndivyo ilivyo hiyo miaka michache katika milele.
11 Kwa hiyo Bwana huwavumilia watu na kuwamiminia huruma zake.
12 Yeye anaona na ajua kuwa mwisho wao ni mbaya kwa hiyo huwajalia msamaha kwa wingi.
13 Mtu humhurumia jirani yake tu, lakini Bwana ana huruma kwa viumbe vyote hai. Yeye huwaonya, huwafunza na kuwafundisha watu. Huwarudisha kama mchungaji arudishapo kundi lake.
14 Yeye huwarehemu wanaokubali nidhamu yake na wanaotamani maamuzi yake.

Wema na kusaidia maskini
15 Mwanangu, usichanganye matendo yako mema na lawama. Unapomsaidia maskini usimhuzunishe kwa maneno yako.
16 Je, umande si unaburudisha wakati wa joto kali? Hivyo neno moja laweza kufaa kuliko zawadi.
17 Neno jema lafaa kuliko zawadi, mtu mkarimu anavyo vyote viwili.
18 Mpumbavu ni mkatili na mwenye matusi. Zawadi ya mtu mchoyo huzima macho.
19 Jifunze kabla ya kusema. Tunza afya yako kabla hujaugua.
20 Jichunguze kabla ya hukumu na siku ile itakapofika, utapata msamaha.
21 Jinyenyekeshe kabla ya kupatwa na ugonjwa. Unapokaribia kutenda dhambi, rudi.
22 Usizuiliwe na chochote kutimiza nadhiri zako, wala usingoje hadi kifo, usamehewe.
23 Jitayarishe kabla ya kuweka nadhiri; wala usiwe kama mtu anayemjaribu Bwana.
24 Fikiri juu ya ghadhabu yake siku utakapokufa, na wakati wa adhabu, atakapogeuzia mbali uso wake.
25 Wakati wa fanaka, fikiria wakati wa njaa. Wakati wa utajiri, fikiria umaskini na ufukara.
26 Tangu asubuhi mpaka jioni, hali hubadilikabadilika. Bwana aweza kugeuza haraka hali za viumbe vyote.
27 Mwenye hekima ni mwangalifu katika kila kitu. Anapokabiliwa na dhambi huchukua hadhari asikosee.
28 Kila mwenye akili anajua hekima, na humsifu yeyote anayeipata.
29 Watu wanaoelewa misemo wanapata kuwa na hekima; nao hububujika methali zifaazo.

Kujichunguza mwenyewe
30 Usizifuate tamaa zako mbaya, bali zuia uchu wako.
31 Ukijiachia kufurahia tamaa mbaya, utakuwa kitu cha kuchekwa na maadui zako.
32 Usijitumbukize katika anasa kubwa, usije ukafilisika kwa gharama zake.
33 Usiwe muflisi kukopa fedha za karamu wakati wewe huna chochote mfukoni.

Generic placeholder image