1

Sifa kwa Hekima
1 Hekima yote hutoka kwa Bwana, nayo imo kwake hata milele.
2 Nani awezaye kuuhesabu mchanga wa pwani au matone ya mvua? Nani awezaye kuzihesabu siku za milele?
3 Je, kimo cha mbingu ni kiasi gani? Je, upana wa dunia ni kiasi gani? Je, kina cha bahari ni kiasi gani? Nani aujuaye umaarufu wa Hekima? Nani awezaye kuyajibu maswali haya?
4 Hekima iliumbwa kabla ya vitu vyote, busara ilikuwako tangu zama zote. [ 5Chanzo cha hekima ni neno la Mungu aliye juu; njia zake ni amri za milele.]
6 Nani aliyeoneshwa kitovu cha Hekima? Nani anafahamu mafumbo ya Hekima? [ 7Ujuzi wa hekima alijulishwa nani? Na uzoefu wake mwingi nani aliyepata kuuelewa?]
8 Yuko mmoja tu mwenye hekima wa kutisha sana, ameketi katika kiti chake cha enzi - ndiye Bwana.
9 Bwana mwenyewe ndiye aliyemuumba Hekima; yeye ndiye aliyemwona na kumpima, na kumjaza katika kazi zake zote.
10 Hekima yumo katika kila kiumbe kadiri atoavyo Mungu; Mungu humgawia kila mtu ampendaye.
11 Kumcha Bwana huleta fahari na sifa, huleta furaha na taji ya shangwe.
12 Kumcha Bwana kwaufurahisha moyo, kwaleta shangwe, furaha na maisha marefu.
13 Amchaye Bwana atafanikiwa mwisho wake; siku ya kufa kwake atabarikiwa.
14 Kumcha Bwana ni mwanzo wa Hekima, Hekima ameumbwa na waaminifu tangu tumboni mwa mama.
15 Amejiwekea msingi wa kudumu kati ya watu, na vizazi vijavyo vitamtegemea Hekima.
16 Kumcha Bwana ni ukamilifu wa hekima, Hekima huwatosheleza watu kwa matunda yake.
17 Huzijaza nyumba zao bidhaa zote wanazohitaji na bohari zao mazao yake.
18 Kumcha Bwana ni kuvikwa taji la hekima, Hekima huleta amani na afya nzuri.
19 Bwana alimwona na kumpima, alinyesha duniani maarifa na utambuzi, na kuwapa fahari wale wanaomshikilia.
20 Kumcha Bwana ni kitovu cha Hekima, na matawi yake ni maisha marefu.
[21 Kumheshimu Bwana huondoa dhambi; panapopatikana uchaji wa Bwana, huondosha hasira.]
22 Hasira isiyo halali haikubaliki, maana hasira husababisha maangamizi ya mtu.
23 Mvumilivu husubiri hadi wakati ufaao, na hatimaye furaha itambubujikia.
24 Huyo huzuia maneno yake hadi wakati ufaao, ndipo watu wengi wataisifu busara yake.
25 Bohari za Hekima zimejaa misemo ya busara, lakini uchaji ni chukizo kwa mwenye dhambi.
26 Ukitaka hekima zishike amri, naye Bwana atakupa hekima,
27 Maana kumcha Bwana ni hekima na nidhamu, naye hupendezwa na uaminifu na upole.
28 Usitupilie mbali kumcha Bwana, wala usimwendee kwa moyo mdanganyifu.
29 Usiwe mnafiki mbele ya watu; uuchunge mdomo wako.
30 Usijitukuze, la sivyo utaanguka na kujiletea aibu wewe mwenyewe. Bwana atazifunua siri zako na kukuangusha mbele ya jumuiya, kwa kuwa hukumwendea Bwana kwa uchaji, na moyo wako ulikuwa umejaa udanganyifu.

Generic placeholder image