10

1 Mtawala mwenye busara huwaelimisha watu wake, utawala wa mtu mwenye akili una utaratibu mzuri.
2 Alivyo mtawala, ndivyo walivyo na maofisa wake; alivyo mkuu ndivyo walivyo na wakazi wa nchi yake.
3 Mfalme asiye na nidhamu ni maangamizi kwa watu wake; fanaka ya mji yatokana na maarifa ya viongozi wake.
4 Utawala wa dunia uko mikononi mwa Bwana, yeye humweka mtawala afaaye kwa wakati wake.
5 Ufanisi wa binadamu umo mikononi mwa Bwana. Bwana ndiye ampaye heshima mwandishi.

Kiburi
6 Usichukizwe na kila kosa la jirani yako, wala usifanye chochote kwa mkikimkiki wa ghadhabu.
7 Kiburi huchukiwa na Mungu na binadamu; udhalimu ni jambo la kuchukiza kwa wote wawili.
8 Kwa sababu ya udhalimu, kiburi na kupenda utajiri, mamlaka ya taifa moja huchukuliwa na taifa lingine.
9 Je, mtu aliye vumbi na majivu atajivunia nini? Hata alipo hai matumbo yake yananuka.
10 Ugonjwa wa muda mrefu humduwaza daktari, leo ni mfalme kesho ni maiti.
11 Maana yanayowapata wote katika kifo ni sawa: Wadudu, wanyama wakali na minyoo.
12 Mwanzo wa kiburi ni kumwacha Bwana na kuupindua moyo wake mbali na muumbaji wake.
13 Maana chanzo cha kiburi ni dhambi na mtu anayeambatana nacho atabubujika uchafu. Ndiyo maana Bwana huwaletea adhabu wasiyoitazamia watu wa namna hiyo na kuwaangamiza kabisa.
14 Bwana amewaondoa wakuu kwenye viti vyao vya enzi, na mahali pao amewaketisha wanyenyekevu.
15 Bwana amewangoa wenye kiburi na mizizi yao, na mahali pao amewaweka wanyenyekevu.
16 Bwana amezifuta nchi za mataifa duniani, na huyaangamiza hadi kwenye misingi ya dunia.
17 Mataifa mengine ameyaondoa na kuyaangamiza, na kufuta kumbukumbu lao duniani.
18 Kiburi hakikuumbwa kwa ajili ya watu, wala ghadhabu kwa ajili ya binadamu.

Watu wa kuheshimiwa
19 Viumbe gani vinavyostahili heshima? Binadamu. Viumbe gani vinavyostahili heshima? Wale wamchao Bwana. Viumbe gani visivyostahili heshima? Binadamu. Viumbe gani visivyostahili heshima? Wanaovunja amri.
20 Kati ya ndugu mkubwa wao anastahili heshima. Wanaomcha Mungu hustahili heshima mbele yake. [
21 Kumcha Mungu ni mwanzo wa mafanikio; lakini ukaidi na kiburi ni mwanzo wa kutofanikiwa.]
22 Matajiri, waheshimiwa na maskini, wajivunie kumcha Bwana.
23 Si vema kumdharau mtu aliye maskini lakini ana akili, wala si vizuri kumheshimu mwenye dhambi.
24 Mtawala, hakimu na mwenye cheo ni wa kuheshimiwa, lakini anayemcha Mungu ni mkuu kuliko hao wote.
25 Mtumwa mwenye hekima atahudumiwa na watu huru; na mwenye busara hatanungunika juu yake.

Kujishusha na kujiheshimu
26 Usijioneshe kuwa mtaalamu ufanyapo kazi yako, wala usijisifu wakati una taabu.
27 Afadhali mtu mwenye bidii kazini na ana kila kitu, kuliko mtu anayezurura akijigamba na hana chakula.
28 Mwanangu, jisifu kwa unyenyekevu, na ujione wewe mwenyewe ustahilivyo.
29 Mtu anayejipatiliza mwenyewe nani atamwona hana hatia? Nani atakayemheshimu mtu anayejidharau mwenyewe?
30 Maskini huweza kuheshimiwa kwa maarifa yake; na tajiri kwa utajiri alio nao.
31 Anayeheshimiwa akiwa maskini bila shaka ataheshimiwa zaidi akiwa tajiri! Anayedharauliwa akiwa tajiri bila shaka atadharauliwa zaidi akiwa maskini!

Generic placeholder image