12

1 Ukitaka kutenda wema chagua mtu wa kumtendea; nawe utapata shukrani kwa wema wako.
2 Mtendee wema mcha Mungu nawe utatuzwa; utatuzwa na mtu huyo, au hakika na Mungu Mkuu.
3 Hakuna jema litakalomjia mtu anayedumu katika uovu, au mtu ambaye anakataa kutoa zaka.
4 Wape msaada watu wamchao Mungu, lakini usiwasaidie wenye dhambi.
5 Watendee wema watu wanyenyekevu lakini usiwape kitu wasiomcha Mungu. Usiwape chakula chochote kile, la sivyo watakitumia kukuangusha; nawe, ukalipwa uovu maradufu kwa wema uliowatendea hao.
6 Hata Mungu Mkuu huwachukia wenye dhambi, naye atawaadhibu hao wasiomcha Mungu.
7 Mpe msaada mtu mwema, lakini usimsaidie mwenye dhambi.
8 Rafiki haonekani wakati wa fanaka; na katika shida hutakosa kumjua adui ni nani.
9 Mtu anapofanikiwa maadui zake huhuzunika, lakini katika shida hata rafiki yake hujitenga naye.
10 Kamwe usimwamini adui; uovu wake uko kama kutu ya shaba.
11 Hata kama ananyenyekea na kuinama mbele yako jichunge na kuchukua tahadhari dhidi yake. Yeye ni kama kioo kinachopata kutu kama huendelei kukisafisha.
12 Usimweke adui karibu nawe, la sivyo atakupindua na kuchukua mahali pako. Usimkalishe kwenye mkono wako wa kulia la sivyo, atachukua kiti chako cha heshima; na mwishowe utatambua ukweli wa maneno yangu, nawe utajuta kutokana na hayo niliyosema.
13 Mchezea nyoka akiumwa hahurumiwi na mtu yeyote! Kadhalika na mtu anayewakaribia wanyama wakali!
14 Hivyo, hakuna amhurumiaye anayeshiriki na wenye dhambi na kujihusisha na dhambi zake.
15 Mwenye dhambi atakaa nawe kwa kitambo tu, lakini ukipatwa na matatizo atakukimbia.
16 Adui ataongea nawe maneno matamu, lakini moyoni mwake atapanga kukutupa shimoni. Adui atatoa machozi mengimengi, lakini akipata nafasi, atatimiza haja yake ya kukuua.
17 Ukipatwa na maafa utamkuta hapo anakungojea, akijidai kwamba anakusaidia, atakutegea kukumaliza.
18 Atatikisa kichwa na kupiga makofi; atanongoneza mengi na kuwa mtu mwingine kabisa.

Generic placeholder image