21

Dhambi
1 Mwanangu, je, umetenda dhambi? Usitende tena. Lakini omba msamaha kwa yale uliyotenda.
2 Ikimbie dhambi kama kumkimbia nyoka; maana ukimsogelea nyoka utaumwa. Meno ya dhambi ni kama ya simba. Dhambi hufisha maisha ya watu.
3 Uvunjaji sheria ni kama panga kali kuwili; ukikujeruhi, mtu hawezi kutibiwa na kupona.
4 Vitisho na ukatili huharibu utajiri; nyumba ya mwenye kiburi itakuwa mahame.
5 Dua la maskini husikika kwa Mungu, na uamuzi wake Mungu huwasili haraka.
6 Anayekataa kukosolewa anatembea katika dhambi, lakini anayemcha Bwana atatubu moyoni mwake.
7 Mtu hodari wa kusema hujulikana kwa mbali, ukakosea, mwenye busara hutambua.
8 Ajengaye nyumba yake kwa fedha ya wengine, ni kama anayekusanya mawe ya kaburi lake.
9 Mkutano wa waovu ni kama kamba ya kitani, mwishoni mwao ni mwali wa moto mkali.
10 Njia ya wenye dhambi imetengenezwa vizuri, lakini mwisho wake ni kwenye shimo la kuzimu.

Hekima na upumbavu
11 Yeyote ashikaye sheria huzitawala fikira zake; hekima ni ukamilifu wa kumcha Bwana.
12 Mtu asiye na akili hafundishiki. Lakini kuna kuwa na akili ambako huongeza uchungu.
13 Maarifa ya mwenye hekima yataongezeka kama mafuriko, Na mawaidha yake kama chemchemi inayobubujika maji.
14 Akili ya mpumbavu ni kama gudulia lililopasuka: Kamwe haiwezi kushika maarifa.
15 Mwenye maarifa akisikia neno la hekima atalisifu na kuliongezea zaidi, lakini mpotovu akilisikia hulidhihaki, na kulitupa mbali kabisa.
16 Mazungumzo ya mpumbavu ni kama mzigo safarini; lakini furaha hupatikana katika maneno ya mwenye akili.
17 Katika mkutano watu hutafuta mawazo ya mwenye busara; nao huyatafakari maneno yake moyoni mwao.
18 Kwa mpumbavu hekima ni kama nyumba iliyoanguka; na maarifa ya mjinga ni maneno yasiyo na mpango.
19 Kwa mpumbavu elimu ni kama pingu miguuni, ni kama pingu kwenye mkono wa kulia.
20 Mpumbavu hucheka kwa sauti, hali mwenye busara hutabasamu tu.
21 Kwa mwenye hekima elimu ni kama taji ya dhahabu; ni kama kikuku kwenye mkono wa kulia.
22 Mpumbavu huharakisha kuingia nyumbani kwa mtu; lakini mwenye busara hungojea mlangoni kwa heshima.
23 Mtu asiye na nidhamu huchungulia ndani, lakini mwenye adabu zake hungoja nje.
24 Ni utovu wa adabu kusikiliza mlangoni mwa watu, kwa wenye busara kufanya hivyo ni aibu.
25 Wafidhuli hupenda kurudia waliyosema wengine, lakini wenye busara maneno yao yana uzito.
26 Wazo la wapumbavu liko mdomoni mwao, lakini wanachosema wenye hekima hutoka akilini mwao.
27 Mtu mbaya anapomlaani Shetani, anajilaani yeye mwenyewe.
28 Mteti huchafua nafsi yake mwenyewe; naye huchukiwa na majirani zake.

Generic placeholder image