43

Jua
1 Fahari ya huko juu ni uangavu wa anga lake; anga laonekana kumetameta kwa fahari yake.
2 Jua litokezapo linatangaza likingaa. Hilo ni kitu cha ajabu alichoumba Mungu Mkuu.
3 Mchana laikausha ardhi, nani awezaye kustahimili joto lake?
4 Mtu huchochea tanuri na kusikia joto lake, lakini jua huichoma milima mara tatu zaidi. Jua hupuliza mionzi yake ya moto, na miali yake mikali hupofusha macho.
5 Jinsi gani alivyo mkuu Bwana aliyeliumba, na ambaye kwa amri yake laendelea na mkondo wake.

Mwezi
6 Vilevile mwezi huangaza kwa wakati wake, nao ni alama ya milele; huongoza nyakati na majira.
7 Nyakati za sikukuu hutambuliwa kwa mwezi; mwanga wake huwa mkubwa halafu hupungua.
8 “Mwezi” wa kalenda jina lake latokana na mwezi, hukua kwa namna ya ajabu katika vipindi vyake; wenyewe ni ishara ya majeshi ya angani ukingaa katika anga la mbinguni.

Nyota
9 Mngao wa nyota unaonesha uzuri wa anga mapambo mazuri sana katika mbingu za juu za Bwana.
10 Kwa amri yake yeye Mtakatifu zinasimama mahali zilipopangiwa; kamwe hazikiuki jukumu lao la ulinzi.

Upinde wa mvua
11 Tazama upinde wa mvua, umsifu yeye aliyeuumba! Upinde wa mvua ni mzuri mno kwa mngao wake!
12 Hulizingira anga kwa nusu mzingo wake mzuri, mikono ya Mungu Mkuu imeutandaza.

Maajabu ya maumbile
13 Kwa amri yake Bwana hupeleka theluji, na umeme humulika anapoamuru.
14 Kadhalika ghala zake hufunguka, mawingu yakaruka kutoka humo kama ndege.
15 Kwa ukuu wake huyakusanya mawingu, na kuipasua barafu ikawa mvua ya mawe.
16 Atokeapo, milima hutetemeshwa, kwa kutaka kwake upepo wa kusi huvuma.
17 Sauti yake ya ngurumo huikemea nchi, kadhalika na upepo wa kaskazi na kimbunga. Huitawanya theluji ikashuka chini kama ndege, kama vile nzige wanaotua.
18 Tunashangaa kuona uzuri wa weupe wake, na kustaajabia kuanguka kwake.
19 Hutawanya ukungu juu ya nchi kama chumvi, na unapoganda huweko vitu vilivyochongoka kama miiba.
20 Huvumisha upepo baridi wa kaskazi, barafu ikaganda juu ya maji, ikafunika madimbwi yote ya maji, ikiwa kama ngao ya kujikingia.
21 Huiteketeza milima na kuchoma nyika, akazinyausha nyasi changa kama kwa moto.
22 Lakini ukungu hurekebisha tena kila kitu, umande unapotokea na kuburudisha.
23 Kwa hekima yake aliituliza bahari kuu, na kuweka huko visiwa.
24 Wanaosafiri baharini husimulia hatari zake, nasi tunashangaa juu ya hayo tunayosikia.
25 Baharini mna viumbe vya ajabu na vya kushangaza, viumbe vikubwa mno na aina zote za viumbe hai.
26 Bwana humwezesha kila mjumbe wake kufaulu, kwa neno lake kila kiumbe hushikishwa pamoja.
27 Ingawa tunasema mengi, hatuwezi kufikia mwisho wao, kwa kifupi: “Bwana ni kila kitu.”
28 Tupate wapi nguvu ya kumsifu? Maana yeye ni mkuu kuliko kazi zake zote.
29 Bwana ni wa kutisha na mkuu sana, nguvu zake ni za ajabu mno.
30 Unapomsifu Bwana, msifu kadiri uwezavyo, maana yeye, anastahili zaidi ya hayo yote. Unapomtukuza, mtukuze kwa nguvu zako zote. Wala usichoke maana huwezi kumsifu yeye ipasavyo.
31 Nani aliyemwona, akaweza kueleza alivyo? Au, nani awezaye kumtukuza ipasavyo?
32 Maajabu mengi makuu kuliko haya, yamefichika, maana tumeziona tu kazi zake chache.
33 Maana Bwana amefanya vitu vyote, akawapa heshima wale wamchao.

Generic placeholder image