16

Mungu atawaadhibu wenye dhambi
1 Usitamani kuwa na watoto wengi wasio na faida; wala kujivunia watoto wa kiume wasiomcha Mungu.
2 Wakiongezeka usifurahi kwa sababu yao, isipokuwa kama wanamcha Bwana.
3 Usiwe na imani juu ya kuendelea kwao kuishi; usitegemee wingi wao. Maana, mtoto mmoja ni bora kuliko elfu; ni afadhali kufa bila mtoto, kuliko kuwa na watoto wasiomcha Mungu.
4 Mji utajaa watu kwa busara ya mtu mmoja, lakini kwa kabila moja la wabaya utabaki mtupu.
5 Macho yangu yameona mambo mengi kama haya; masikio yangu yamesikia mambo ya ajabu kuliko hayo.
6 Moto utawashwa katika kusanyiko la wenye dhambi, ghadhabu iliwashwa katika taifa lililoasi.
7 Yale majitu ya zamani hakuyasamehe, majitu ambayo kwa kutegemea nguvu zao yaliasi.
8 Mungu hakuwahurumia jirani za Loti, watu ambao alichukizwa na kiburi chao.
9 Hakulionea huruma taifa lililopangiwa kuangamizwa, taifa lililofutiliwa mbali kwa sababu ya dhambi zake;
10 hata wale wanajeshi 600,000 wa miguu ambao walikusanyika pamoja, wakaasi kwa kiburi chao.
11 Hata kama kuna mtu mmoja mwenye kiburi, itakuwa ajabu kama hataadhibiwa. Maana Bwana ni mwenye huruma na ghadhabu. Yeye ana nguvu kuu ya kusamehe na huwaka hasira; na wale wasiotubu anawamwagia ghadhabu yake.
12 Kama zilivyo kuu huruma zake ndivyo na karipio lake. Yeye humhukumu mtu kulingana na matendo yake.
13 Mwenye dhambi hataweza kutoroka na alichonyakua; na tazamio la wanaomcha Mungu halitakuwa bure.
14 Mwadilifu atapokea anayostahili, kila mtu atapokea kulingana na matendo yake. [ 15Bwana alimfanya Farao awe na kiburi hata asimkiri Bwana; ili ulimwengu ujue kazi za Bwana. 16Huruma yake ni wazi kwa viumbe vyote; alitenga kati ya mwanga wake na giza kwa kamba ya kupimia.]
17 Usiseme, “Nitajificha mbali na Bwana; na hamna yeyote huko juu atakayenikumbuka! Kati ya watu wengi hivyo sitajulikana, maana, nafsi yangu ni kitu gani kati ya viumbe visivyohesabika?”
18 Tazama, mbingu na mbingu za juu kabisa, kuzimu na dunia, vyote vitatetemeka, wakati Bwana atakapokuja.
19 Milima na misingi ya dunia hutetemeka, wakati Bwana anapoviangalia.
20 Lakini hakuna binadamu anayefikiri hayo; ni nani awezaye kuelewa njia za Mungu?
21 Usiseme: “Nikitenda dhambi hakuna anionaye. Nikitenda hayo katika siri kuu nani atajua?
22 Na nikitenda mema nani atayataja? Nani anangojea apewe taarifa? Yeye hukawia mno kutekeleza agano lake.”
23 Ndivyo afikiriavyo mtu asiye na akili; mtu mjinga aliyepotoshwa hufikiri kipumbavu.

Hekima ya Mungu katika maumbile
24 Mwanangu, nisikilize ujifunze maarifa. Tega sikio usikie maneno yangu.
25 Nitakupa mafunzo mazitomazito, nitakufundisha maarifa kwa usahihi.
26 Mungu alipoumba kazi zake mwanzoni alizifanya ziwepo na kuzipa mpango,
27 akazipa mpango wa kufuata milele, tangu mwanzo wake na vizazi vyote. Hivyo hazitindikiwi wala kuchoka na haziachi kutekeleza wajibu wao.
28 Hakuna hata mojawapo inayosongana na nyingine na wala haziachi kutii neno lake Mungu.
29 Baada ya hayo yote Bwana aliiangalia dunia akaijaza vitu vyake vizuri.
30 Aliifunika dunia kwa kila aina ya viumbe, ambavyo vitakufa na kurudi udongoni.

Generic placeholder image