5

Usiwe na majivuno
1 Usitegemee mali zako, wala usiseme, “Nina mali ya kutosha.”
2 Usiongozwe na tamaa yako na nguvu yako, katika kufuata tamaa za moyo wako.
3 Usiseme, “Nani atanishinda?” maana hakika Bwana atakuadhibu.
4 Usiseme, “Nimetenda dhambi, lakini nimepata balaa gani?” maana Bwana hakasiriki upesi.
5 Usitegemee kupata msamaha, hata kuongeza dhambi juu ya dhambi.
6 Usiseme, “Huruma yake ni kubwa; yeye atanisamehe dhambi zangu nyingi.” Kumbuka, yeye ana huruma na ghadhabu, na hasira yake huwakumba wenye dhambi.
7 Usichelewe kumrudia Bwana, wala usiahirishe kurudi siku hata siku. Maana ghadhabu ya Bwana itakuwakia ghafla, na wakati wa hukumu utaangamia.
8 Usitegemee mali ya udanganyifu; maana haitakufaa chochote siku ya balaa.

Uaminifu na kujitawala
9 Usipepete nafaka kwa kila upepo, wala kufuata asemacho mtu: Hiyo ndiyo desturi ya mwenye dhambi mdanganyifu.
10 Uwe na msimamo thabiti katika nia yako, na usiwe kigeugeu katika maneno yako.
11 Uwe mwepesi kusikiliza, lakini uwe mwangalifu katika kutoa jibu.
12 Kama unajua jambo hilo, mjibu jirani yako, la hujui, basi usijibu.
13 Sifa na aibu vyote hutokana na kusema. ulimi wa mtu waweza kumwangamiza.
14 Usikubali kujipatia sifa kwa kuteta, usikubali kusema kitakachowahatarisha wengine. Maana kama vile aibu humjia mwizi, ndivyo hukumu kali itakavyompata mdanganyifu.
15 Usikosee katika jambo lolote kubwa au dogo, wala usiwe adui pale unapotakiwa kuwa rafiki.

Generic placeholder image