33

1 Hakuna baa lolote litakalompata mtu amchaye Bwana; wakati wa majaribu Bwana atamwokoa tena na tena.
2 Mwenye hekima hataichukia sheria, lakini mnafiki juu ya sheria ni kama mashua kwenye mawimbi.
3 Mwenye busara atakuwa na imani na sheria, kwake sheria ni ya kutegemewa kama kauli ya Mungu.
4 Tayarisha utakachosema nawe utasikilizwa; panga pamoja unayoyajua kisha ujibu.
5 Moyo wa mpumbavu ni kama gurudumu la mkokoteni, na mawazo yake kama kizungukio.
6 Rafiki mwenye mizaha ni kama farasi; kila anayempanda farasi hutoa sauti.

Watu hawalingani
7 Kwa nini siku moja ni bora kuliko nyingine hali zote zinapata mwanga wake kutoka kwa jua?
8 Bwana ndiye aliyeamua kuzitofautisha, na kuweka majira mbalimbali na sikukuu.
9 Siku nyingine alizikuza na kuzitakasa, na nyingine alizifanya ziwe za kawaida tu.
10 Binadamu wote wametoka udongoni, naye Adamu aliumbwa kutoka mavumbini.
11 Lakini, Bwana kwa hekima yake kamili aliwatofautisha, na kila mmoja wao akampa jukumu tofauti.
12 Baadhi yao aliwabariki na kuwakuza, baadhi aliwafanya watakatifu na kuwaweka karibu naye. Lakini wengine aliwalaani na kuwashusha, akawaondoa kutoka mahali pao.
13 Kama udongo mikononi mwa mfinyanzi ambaye huufinyanga atakavyo, ndivyo walivyo binadamu mikononi mwake aliyewaumba: Yeye huwafanya kama anavyoamua.
14 Wema ni kinyume cha uovu, na uhai ni kinyume cha kifo, ndivyo na mwenye dhambi ni kinyume cha mcha Mungu.
15 Angalia kazi zote za Mungu Mkuu: Ziko mbilimbili, kimoja kinyume cha kingine.
16 Mimi, nimekuwa wa mwisho kuyaangalia hayo, kama mtu anayeokota zabibu baada ya wavunaji kupita.
17 Lakini Bwana amenibariki sana, nikawazidi wote; kama vile mvunazabibu nimejaza kinu cha kusindikia.
18 Kumbuka sikufanya kazi kwa ajili yangu tu, bali kwa ajili ya wote wanaotaka kujifunza.
19 Nisikilizeni enyi wakuu kati ya watu; nanyi viongozi wa jumuiya, nisikilizeni.

Daima uwe huru
20 Muda wote uishipo usimwachie mtoto, mke, ndugu au rafiki akutawale; usimpe mtu mwingine mali yako, usije ukabadili nia na kuomba urudishiwe.
21 Ungali bado hai, unapumua, usikubali mtu mwingine achukue nafasi yako.
22 Maana ni afadhali watoto wako wakutegemee, kuliko wewe kuwategemea wao.
23 Fanya kila kitu ufanyacho vizuri kabisa, usiitie dosari heshima yako.
24 Mwisho wa maisha yako, wakati wa saa yako ya mwisho, gawa mali yako.

Watumwa
25 Nyasi, mzigo na kiboko kwa punda, chakula, nidhamu na kazi kwa mtumwa.
26 Mpe mtumwa wako kazi nawe utapata pumziko, mwache bila kazi naye atataka uhuru.
27 Mtiishe mnyama kwa nira na lijamu, na mtumwa mwovu kwa mateso.
28 Mpe kazi ili asiwe mvivu, maana uvivu huwafunza watu uovu mwingi.
29 Mpe kazi kama inavyostahili kwako, na kama hakutii, mfunge minyororo.
30 Usimtendee mtu yeyote bila kiasi, wala usifanye chochote bila busara.
31 Ukiwa na mtumwa na awe kama wewe, kwa sababu umemnunua kwa jasho lako.
32 Ukiwa na mtumwa, mtendee kama ndugu yako, maana utamhitaji kama unavyohitaji roho yako.
33 Ukimtendea vibaya akakukimbia, utafuata njia ipi kumtafuta?

Generic placeholder image