50

Simoni
1 Aliyekuwa mkuu wa ndugu zake na fahari ya watu wake, ni Simoni, kuhani mkuu, mwana wa Onia. Katika maisha yake alilijenga upya hekalu, na kulijengea ngome.
2 Aliweka msingi wa kuta mbili za ua wa hekalu.
3 Wakati wake kisima cha maji kilichimbwa, hifadhi ya maji kubwa kama bahari.
4 Alifikiria namna ya kuwaokoa watu wasiangamie, akauimarisha mji kuukinga na mashambulizi.
5 Jinsi gani alivyoheshimika akizungukwa na watu, alipokuwa akitoka mahali patakatifu ndani.
6 Alikuwa kama nyota ya asubuhi mawinguni, alikuwa kama mwezi mpevu.
7 Alikuwa kama jua linapoangaza juu ya hekalu la Mungu Mkuu, kama upinde wa mvua unaongara katika mawingu.
8 Alikuwa kama waridi wakati wa mazao ya kwanza, kama yungiyungi kando ya kijito, kama chipukizi mlimani Lebanoni wakati wa kiangazi,
9 kama ubani katika moto ndani ya chetezo, kama chombo cha dhahabu iliyofuliwa, kilichopambwa kwa kila aina ya mawe ya thamani.
10 Alikuwa kama mzeituni unapotoa matunda yake, kama mberoshi mrefu mpaka mawinguni.
11 Alipovaa mavazi yake ya fahari, alipokwenda kwenye madhabahu matakatifu, akiwa amevalia mavazi yake kikamilifu, aliufanya ukumbi wa hekalu uwe na utukufu.
12 Makuhani walipompa mafungu yake ya tambiko, akiwa amesimama karibu na madhabahu, amezungukwa na ndugu zake kama taji, alikuwa kama mwerezi mchanga mlimani Lebanoni. Ndugu zake walimzunguka kama mtende na matawi yake,
13 yaani wazawa wote wa Aroni, wakiwa wamevaa mavazi yao yenye utukufu, wakiwa na tambiko za matoleo kwa Bwana mikononi, wamesimama mbele ya jumuiya yote ya Israeli.
14 Alipomaliza huduma yake madhabahuni, na kuzipanga tambiko za Mungu Mkuu, Mwenye Nguvu,
15 alinyosha mkono akachukua kikombe, akaimimina divai kwenye msingi wa madhabahu, ikiwa ni tambiko ya kinywaji, impendezayo Mungu Mkuu, mfalme wa wote.
16 Kisha wazawa wa Aroni, walipiga kelele, na kupiga tarumbeta zao za fedha, wakitangaza kuweko kwake Mungu Mkuu.
17 Ndipo watu wote pamoja walifanya haraka, wakasujudu na kumwabudu Bwana wao, Mungu Mwenye Nguvu, Mungu Mkuu.
18 Nao waimbaji wakamsifu kwa sauti zao, kwa muziki mtamu na tuni kamili.
19 Nao watu wakamsihi Bwana Mungu Mkuu, wakamwomba yeye mwenye huruma mpaka utaratibu wa kumwabudu Bwana ulipokwisha. Ndivyo walivyokamilisha ibada yake.
20 Kisha Simoni akatoka, akainua mikono yake juu ya jumuiya yote ya Israeli, ili kutamka baraka za Bwana kwa kinywa chake, na kulitukuza jina lake.
21 Nao wakasujudu kwa mara ya pili, kupokea baraka za Mungu aliye juu ya yote.

Mausia
22 Sasa msifuni Mungu wa wote, ambaye hufanya makuu kila mahali; ambaye hutunza maisha yetu tangu kuzaliwa, na kututendea kadiri ya huruma zake.
23 Na atupe furaha ya moyoni, na kutujalia amani siku zetu katika Israeli kama vile nyakati za kale.
24 Huruma yake na iwe kati yetu; yeye na atukomboe katika siku zetu.
25 Kuna mataifa mawili ambayo nayachukia, na la tatu halifai hata kuitwa taifa.
26 Wakazi wa mlima Seiri na Wafilisti, na wale watu wapumbavu wanaoishi Shekemu.

Maneno ya mwisho
27 Nimeandika katika kitabu hiki mafundisho ya hekima na maarifa. Mimi ni Yoshua mwana wa Sira mwana wa Eleazari wa Yerusalemu ambaye moyoni mwangu nimebubujika hekima.
28 Heri mtu anayeyatafakari mambo hayo; naye ayawekaye moyoni atapata hekima.
29 Maana atakayeyatenda ataimarika daima, kwa kuwa kumcha Bwana ni uhai.

Generic placeholder image