3

Wajibu wa watoto kwa wazazi
1 Wanangu sikilizeni mawaidha ya baba yenu. Fanyeni ninayowaambia, nanyi mtawekwa salama,
2 maana Bwana amewapa kina baba mamlaka juu ya watoto wao, na kuimarisha uwezo wa kina mama juu ya watoto wao.
3 Anayemheshimu baba yake anajipatia msamaha wa dhambi zake.
4 Anayemheshimu mama yake anajiwekea hazina kubwa.
5 Anayemheshimu baba yake atafurahishwa na watoto wake mwenyewe, na atakapomwomba Bwana, atasikilizwa.
6 Anayemheshimu baba yake atapata maisha marefu, anayempendeza mama yake anamtii Bwana.
7 Mtoto huyo, huwatumikia wazazi wake kama Bwana wake.
8 Mheshimu baba yako kwa maneno na matendo, ili upate baraka kutoka kwake.
9 Maana baraka za baba huimarisha nyumba za watoto, hali laana ya mama huingoa misingi ya nyumba zao.
10 Usijikuze mwenyewe kwa kumdharau baba yako. Maana kumdharau baba yako hakutakuletea faida.
11 Maana fahari ya baba mtu ni fahari ya huyo mtoto, na watoto wasiomheshimu mama yao ni balaa.
12 Mwanangu, mtunze baba yako alipo mzee wala usimhuzunishe muda wote aishipo.
13 Hata akipungukiwa akili, umvumilie. Usimdharau kwa vile wewe una afya na nguvu.
14 Bwana hatasahau wema wako kwa baba yako, utakusaidia kukupatia msamaha wa dhambi zako.
15 Wakati wa taabu Bwana atakumbuka wema wako. Kama umande kwenye jua, dhambi zako zitatoweka.
16 Anayemtupa baba yake anamkufuru Mungu; anayemkasirisha mama yake analaaniwa na Bwana.

Unyenyekevu
17 Mwanangu, uwe mpole katika shughuli zako, nawe utapendwa na wale wanaokubaliwa na Mungu.
18 Kadiri ulivyo mkuu, ndivyo unavyotakiwa kunyenyekea; na hapo utapata kibali cha Bwana. [ 19Wengi hujitukuza na kujiona bora, lakini siri za Mungu hufunuliwa kwa wanyenyekevu. Makala ya Kiebrania: Huruma za Mungu ni kubwa, naye huwafunulia wanyenyekevu siri zake.]
20 Nguvu ya Bwana ni kuu lakini hutukuzwa na wanyenyekevu.
21 Usitafute yaliyo magumu mno kwako, wala kuchunguza yaliyo nje ya uwezo wako.
22 Zingatia yale uliyopangiwa kufanya, huhitaji kujihangaisha juu ya mambo yaliyofichika
23 Usiingilie mambo yanayopita nguvu zako maana hata hayo uliyooneshwa yanapita akili ya binadamu.
24 Maana wengi wamepotoshwa kwa kujiona kuwa wajuzi sana, maoni yao ya utundu yamepotosha akili zao. [ 25Kama huna macho huwezi kuona; usijitakie kuwa na akili kama hunayo.]
26 Mwenye kiburi ataishia vibaya mwishoni; na apendaye hatari ataangamia huko.
27 Mwenye kiburi atalemewa taabu; mwenye dhambi hujirundikia dhambi mfululizo.
28 Mateso ya mwenye kiburi hayana matibabu. Maana uovu umeota na kutia mzizi ndani yake.
29 Mwenye akili atazitafakari methali moyoni mwake; kuwa mtu msikivu ndicho atakacho mwenye busara.

Kuwasaidia maskini
30 Kama vile maji yazimavyo moto mkali ndivyo na sadaka kwa maskini iletavyo msamaha wa dhambi.
31 Amwoneaye huruma mwenzake hufikiria mbele, wakati atakapopata taabu atasaidiwa.

Generic placeholder image