37

1 Kila mtu anaweza kudai, “Mimi pia ni rafiki yako.” Lakini rafiki wengine ni rafiki kwa jina tu.
2 Je, si pigo la kifo ndugu au rafiki akiwa adui?
3 Ee mwelekeo wa uovu, kwa nini umeumbwa hata ukaijaza dunia kwa udanganyifu?
4 Baadhi ya ndugu hufurahia furaha ya rafiki, lakini, wakati wa taabu humwacha.
5 Wengine humsaidia rafiki kwa ajili ya chakula, lakini vita vikitokea, hujikinga wao wenyewe.
6 Usimsahau rafiki yako wa kweli; na unapokuwa tajiri usimfute moyoni mwako.

Washauri
7 Kila mshauri atatoa ushauri, lakini wengine hutoa ushauri kwa faida yao.
8 Uwe mwangalifu juu ya mshauri, ukachunguze kwanza anachotaka, maana huenda anajifikiria yeye mwenyewe tu. Huenda amekwisha fanya mpango dhidi yako.
9 Huweza kusema: “Mambo yote ni sawa”, halafu akasimama mbali kuona yatakayokupata.
10 Usiombe ushauri kwa mtu unayemwonea mashaka, na usimpe ushauri mtu anayekuonea wivu.
11 Usiombe ushauri kwa mwanamke kuhusu mpinzani wake, usiombe ushauri kwa mwoga kuhusu vita, kwa mfanyabiashara kuhusu biashara, kwa mnunuzi kuhusu uuzaji wa mali, kwa mtu bahili kuhusu ukarimu, kwa mtu mkatili kuhusu upole; kwa mtu mvivu kuhusu kazi, kwa kibarua kuhusu kumaliza kazi, au kwa mtumwa mvivu kuhusu kazi ngumu. Usiwajali watu wa namna hiyo, kuhusu jambo la kupata ushauri.
12 Lakini uwe na uhusiano daima na mcha Mungu, ambaye unajua anatii amri, yeye nawe mnapatana, naye atahuzunika nawe ukishindwa.
13 Utegemee sana shauri la moyo wako; maana hakuna aliye mwaminifu kuliko moyo wako.
14 Moyo wa mtu mara nyingi humpa mawaidha mema kuliko yale ya walinzi saba wanaolinda zamu mnarani.
15 Zaidi ya hayo, mwombe Mungu Mkuu ili aiongoze njia yako katika ukweli.

Hekima ya kweli na ya uongo
16 Busara iwe ndio msingi wa kila tendo, na shauri hutangulia shughuli yoyote.
17 Mawazo yote yamo moyoni, na kutoka humo namna nne huonekana:
18 Wema na uovu, uhai na kifo; na mtawala wa hayo daima ni ulimi.
19 Mtu aweza kuwa na busara na mwalimu wa wengi, lakini asiwe na faida kwake mwenyewe.
20 Mtu aliye hodari wa kusema aweza kuchukiwa, hata akakosa chakula kabisa,
21 maana hakupewa neema na Bwana, kwa vile hana hekima yoyote.
22 Mwingine ana hekima kwa faida yake mwenyewe, na maneno yake akayaona yeye mwenyewe kuwa hakika.
23 Mwenye hekima atawafunza watu wake, na matokeo ya maarifa yake yatakuwa hakika.
24 Mwenye hekima atapewa sifa kwa wingi, na wote watakaomwona watamwita mwenye bahati.
25 Siku za maisha ya mtu zimehesabiwa, lakini siku za Israeli hazihesabiki.
26 Mwenye hekima atajipatia heshima kwa watu wake, na jina lake litadumu milele.

Kuwa na kiasi
27 Mwanangu, jipime nafsi yako ungali hai; ona ni kitu gani kibaya kwako, ukiepe.
28 Maana si kila kitu kinafaa kwa kila mtu, wala si kila mtu anafurahia kila kitu.
29 Usiwe mwenye uchu wa kila anasa, wala usiwe mtumwa wa chakula.
30 Maana kula mno huleta ugonjwa, ulafi huleta kichefuchefu.
31 Wengi wamekufa kwa sababu ya ulafi, anayekwepa ulafi, atarefusha maisha yake.

Generic placeholder image