27

1 Watu wengi wametenda dhambi kutafuta faida; nayetaka kuwa tajiri yampasa kuchunga macho yake.
2 Kama vile kigingi kilivyoshikiwa imara katika mawe ya nyumba, ndivyo dhambi ilivyoshikiwa imara katika kuuza na kununua.
3 Mtu yeyote asiyezingatia kumcha Bwana, nyumba yake itaangamizwa punde si punde.

Hotuba
4 Ukitikisa chekecheke makapi hubaki, ndivyo na uchafu wa mtu unavyobaki katika mawazo yake.
5 Tanuri hupima kazi za mfinyanzi, ndivyo pia mazungumzo yanavyompima mtu.
6 Matunda huonesha mti ulivyotunzwa, vivyo hivyo maneno ya mtu humjulisha alivyo.
7 Usimsifu mtu ambaye hajaongea kwa vile mtu hupimwa kwa maneno yake.

Uaminifu
8 Ukitaka kuwa mwema utafanikiwa kuwa mwema, na kuuvaa wema kama vazi la sikukuu.
9 Ndege hujumuika na ndege wa aina yao, ndivyo na ukweli unavyoandamana na wale wanaoutekeleza.
10 Kama vile simba anavyootea mawindo, ndivyo na dhambi inavyowaotea watendao uovu.
11 Mazungumzo ya wenye kumcha Mungu ni ya hekima daima, lakini mpumbavu hubadilika kama mwezi.
12 Ukijikuta miongoni mwa wapumbavu ondoka; lakini miongoni mwa wenye busara, kaa.
13 Mazungumzo ya wapumbavu ni kinyaa, na kucheka kwao ni ufisadi wa dhambi.
14 Kuongea kwa watu hao hukufanya ushtuke kabisa, na mabishano yao humfanya mtu azibe masikio.
15 Ugomvi wa wenye majivuno husababisha mauaji, na matusi yao ni aibu kuyasikiliza.

Kutoa siri
16 Anayetoa siri anakosa uaminifu wote, na kamwe hatapata rafiki anayemtaka.
17 Mpende rafiki na uwe na imani naye, lakini kama umetoa siri zake, usiandamane naye tena.
18 Maana, kama mtu anavyomwangamiza adui wewe nawe umeharibu urafiki wa jirani yako.
19 Kama ulivyomwachilia ndege achopoke mkononi mwako, hivyo umemwachilia jirani yako, wala hutaweza kumpata tena.
20 Usimfuate, maana amekwenda mbali sana, amekimbia kama paa aliyenusurika kwenye mtego.
21 Kidonda chaweza kutibiwa, na kutukanwa kusamehewa; lakini aliyetoa siri, asitumaini lolote.

Unafiki
22 Anayepepesa macho anakusudia kutenda maovu, wala hakuna mtu anayeweza kumvumilia.
23 Mtu huyo awapo nawe, anayosema ni matamu, na atayafurahia unayomwambia. Lakini baadaye, atabadilisha usemi wake, na kukunasa kwa maneno yako mwenyewe.
24 Maishani nimeyachukia mambo mengi, lakini mtu kama huyo namchukia kuliko yote, hata Bwana anamchukia mtu kama huyo.
25 Anayetupa jiwe juu angani analitupa kichwani mwake mwenyewe. Apigaye ngumi hujiumiza mwenyewe.
26 Mchimba shimo hutumbukia yeye mwenyewe, na mtega mtego hunaswa mwenyewe.
27 Mtu akitenda uovu, uovu utampata, wala hatajua umetoka wapi.
28 Mwenye majivuno hudhihaki na kudharau, lakini adhabu inamngojea kama simba.
29 Wanaofurahia kuanguka kwa wenye kumcha Mungu, watanaswa katika mtego na maumivu yatawakumba kabla ya kufa kwao.

Chuki
30 Hasira na ghadhabu, yote ni machukizo, na mwenye dhambi atayapata yote hayo.

Generic placeholder image