13

1 Mtu yeyote agusaye lami atachafuka, na anayeshirikiana na mwenye kiburi atakuwa kama yeye.
2 Usikubali kubeba mzigo upitao nguvu zako, usishirikiane na mwenye nguvu na tajiri kuliko wewe. Chungu cha udongo chawezaje kushirikiana na birika la chuma? Kama vikigongana hicho chungu ndicho kitakachovunjika.
3 Tajiri humkosea mtu hata akadiriki kuongeza matusi juu. Lakini maskini akikosa hulazimika kuomba msamaha.
4 Tajiri atakunyonya kila anapopata faida kwako. Lakini unapotaka akusaidie atakuacha hivihivi.
5 Kama una kitu atakaa nawe; atafyonza mali yako bila hata kujali.
6 Anapokuhitaji atakudanganya, atakuchekea na kukupa tumaini. Atakuuliza kwa upole: “Unahitaji chochote?”
7 Atakufanya uone haya kwa makaribisho yake ya chakula; akiisha kukunyonya mara mbili tatu, atakucheka. Kama ukimwona baadaye atajidai hakujui na kukutikisia kichwa chake.
8 Jichunge usije ukapotoshwa; na kufedheheshwa kwa sherehe zako.
9 Ukialikwa na mtu maarufu, uwe mtaratibu; naye atakualika mara nyingi.
10 Usijipeleke kwake kwa pupa, la sivyo atakufukuza. Lakini ukikaa mbali naye sana, atakusahau.
11 Usijidai kuwa sawa naye, wala usisadiki maneno yake mengi. Maana atakupima kwa mazungumzo yake marefu, na anapokucheka, atakuwa anakuchunguza.
12 Mtu asiyeshika siri ni mtu mkatili. Hatasita kukudhuru au kukutia gerezani.
13 Tunza siri zako na uwe mwangalifu, maana unatembea kwenye hatari. [ Ukisikia kitu unapolala amka!
14 Mpende Bwana maisha yako yote na kumwomba akuokoe.]
15 Kila kiumbe hupenda kiumbe cha aina yake, kadhalika na binadamu humpenda binadamu mwenzake.
16 Viumbe vyote hujumuika na aina zao, kadhalika na mtu hujumuika na aliye kama yeye.
17 Mbwamwitu na mwanakondoo wana ushirika gani? Ni vigumu zaidi kushirikisha mwenye dhambi na mcha Mungu!
18 Je, kuna amani yoyote kati ya fisi na mbwa? Na je, kuna amani yoyote kati ya tajiri na fukara?
19 Pundamwitu ni mawindo ya simba; nao maskini ni malisho ya matajiri.
20 Unyenyekevu ni chukizo kwa mtu mwenye kiburi, vivyo hivyo maskini ni chukizo kwa mtu tajiri.
21 Tajiri akitetereka hutegemezwa na rafikize. Lakini maskini akianguka rafikize humsukumia mbali,
22 Tajiri akikosea, wa kumsaidia ni wengi; hata akisema maneno yasiyofaa, humtetea kuwa sawa. Lakini maskini akitetereka watamkaripia, hata kama akiongea kwa busara, hakuna anayemjali.
23 Tajiri akiongea, wote hunyamaza, huyasifu anayoongea hadi mawinguni. Mtu maskini akiongea, watu husema, “Ni nani huyu?” Na akijikwaa, watamsukumiza chini.
24 Utajiri ni mzuri kama hauhusiani na dhambi, na umaskini ni mbaya kwa maoni ya wasiomcha Mungu.
25 Hali ya mtu moyoni husababisha hali yake ya nje: Iwe ya furaha au ya huzuni.
26 Uso mkunjufu ni alama ya furaha moyoni, utaonekana mwenye furaha hata nje. Lakini kuvumbua methali kunahitaji kufikiri sana.

Generic placeholder image