42

Kuona fahari
1 Haya ndiyo mambo ambayo hutaona haya kutenda, wala usitende dhambi kwa kuogopa watu watasema nini:
2 Usione haya kufuata sheria ya Mungu Mkuu na agano lake, usione haya kutoa uamuzi wa haki kuwahukumu wenye hatia.
3 Usione haya kuwajibika na mwenzako wa kazi na msafiri, na kugawana urithi na rafiki.
4 Usione haya kutumia mizani na vipimo halali,
5 kujipatia faida kwa wafanyabiashara, kuwafunza watoto nidhamu ya hali ya juu, kumchapa vikali mtumishi mwovu.
6 Kama mkeo haaminiki, mfiche mambo yako, na penye watu wengi fungia vitu vyako ndani.
7 Chochote unachotoa, ujue idadi na kipimo chake, weka katika maandishi mapato na matumizi.
8 Usione haya kumfunza mjinga na mpumbavu au mzee agombanaye na vijana. Hivyo utakuwa kweli umeelimishwa, nawe utapata kibali mbele ya watu wote.
9 Baba mwenye binti hukesha kwa siri kwa ajili yake; wasiwasi wa baba juu ya binti humzuia kulala.
10 Akiwa bado msichana baba yake anaogopa ataharibiwa, au atapata mimba akiwa bado nyumbani kwake; au akiwa ameolewa baba yake anaogopa kwamba anaweza kuwa tasa.
11 Mchunge sana binti aliye mtundu, la sivyo atakufanya uchekwe na maadui zako, ukawa kioja mjini na mwenye jina baya kwa watu, ukaaibishwa naye mbele ya umati wa watu.

Wanawake
12 Usikodolee macho uzuri wa mtu yeyote, wala kukaa kuzungumza na wanawake.
13 Maana nondo hutoka katika mavazi, na ubaya wa mwanamke hutoka kwa mwanamke.
14 Afadhali uovu wa mwanamume kuliko wema wa mwanamke; mwanamke ndiye asababishaye aibu na fedheha.

Utukufu wa Mungu ulimwenguni
15 Sasa, nitawakumbusha kazi za Bwana, na kutangaza yale niliyoyaona: Kazi za Bwana hufanyika kwa neno lake.
16 Jua hutazama kila kitu chini kwa miali yake, kazi ya Bwana imejaa utukufu wake.
17 Hakuna hata mmoja wa malaika wake Bwana awezaye kutaja matendo yake yote ya ajabu ambayo Bwana Mwenyezi-Mungu ameyaimarisha. ili ulimwengu uwe imara katika utukufu wake.
18 Yeye huchunguza vilindi na mioyo ya watu, na kuiona mipango yao ya hila. Maana Mungu Mkuu anajua elimu yote ile, na anazijua ishara za nyakati.
19 Yeye hutangaza yaliyotukia na yajayo, na kufunua chochote kilichofichika.
20 Hakuna wazo linaloweza kumponyoka, hakuna hata neno moja liwezalo kujificha mbali naye.
21 Yeye amepanga fahari za hekima yake. Yeye ndiye peke yake aliye tangu milele hata milele. Hawezi kuongezewa kitu au kupokonywa kitu; wala hahitaji mtu yeyote kuwa mshauri wake.
22 Jinsi gani zipendezavyo kazi zake! Jinsi gani zingaavyo kuziona!
23 Vitu hivyo vyote vipo na vyadumu milele, na kila vinapohitajiwa humtii kila mara.
24 Viumbe vyote vimepangwa viwiliviwili kila kimoja kikiwa kinyume cha kingine; na hakuna alichofanya kisicho kamili.
25 Kitu kimoja huukamilisha uzuri wa kingine. Nani anaweza kuchoka kuangalia utukufu wake?

Generic placeholder image