35

1 Anayeishika sheria ametoa sadaka nyingi.
2 Anayezifuata amri ametoa sadaka za amani.
3 Anayerudisha shukrani anatoa sadaka ya nafaka safi;
4 naye anayemsaidia maskini anatoa sadaka ya shukrani.
5 Kuachana na uovu kunampendeza Bwana, na kuacha ubaya ni kujiletea upatanisho.
6 Usiende mbele za Bwana mikono mitupu,
7 maana vitu hivi vyote vinatakiwa na amri;
8 sadaka ya mtu mwadilifu huipaka madhabahu mafuta na harufu yake nzuri hupanda mbele ya Mungu Mkuu.
9 Sadaka ya mwadilifu hukubaliwa; nayo haitasahaulika milele.
10 Mtukuze Bwana kwa ukarimu, wala usiwe mchoyo juu ya mazao yako ya kwanza.
11 Zawadi zako zote uzitoe kwa moyo mkunjufu, weka wakfu zaka zako kwa furaha.
12 Mpe Mungu Mkuu kama alivyokupa, uwe mkarimu kwa kadiri ulivyo navyo.
13 Maana Bwana ndiye anayelipa, naye atakulipa mara saba.
14 Usijaribu kumhonga, maana hatapokea,
15 wala usitegemee sadaka ulizopata kwa udanganyifu. Maana Bwana ni hakimu, wala hana upendeleo.

Haki ya Mungu
16 Bwana hataonesha upendeleo kwa maskini; aliyekosewa anapomwomba, humsikiliza.
17 Yeye hayapuuzi maombi ya yatima, wala maombi ya mjane anapomwambia kisa chake.
18 Machozi ya mjane hutiririka mashavuni mwake,
19 yakimshtaki mtu aliyesababisha mateso yake.
20 Anayemtumikia Bwana na kumpendeza atakubaliwa naye, sala yake itafika mbinguni.
21 Sala ya mnyenyekevu huyapenya mawingu, nayo haitasimama mpaka imemfikia Bwana. Hataacha kuomba mpaka Mungu Mkuu amemjibu,
22 akamwokoa mwadilifu na kutoa hukumu. Bwana hatakawia wala hatawaonesha uvumilivu, mpaka atakapowaponda wasio na huruma,
23 na huyalipiza kisasi mataifa maovu; mpaka awaangamize wenye kiburi wengi na kuvunjilia mbali utawala wa waovu.
24 Atawalipiza kisasi watu kadiri ya matendo yao, kila mtu kulingana na mipango yake,
25 mpaka atakapoamua kisa cha watu wake na kuwafanya wafurahi kwa sababu ya huruma yake.
26 Nyakati za shida, huruma yake hupokelewa kwa furaha kama mvua wakati wa ukame.

Generic placeholder image