20

Wakati wa kufaa kuongea
1 Mtu anaweza kukaripiwa wakati usiofaa; una ukimya ambao huonesha mtu ana hekima.
2 Afadhali zaidi kumwonya mtu kuliko kukaa na hasira.
3 Anayekiri kosa lake anajiepusha na balaa.
4 Kama vile towashi anayetaka kumnajisi msichana ndivyo alivyo mtu anayetaka kutekeleza maamuzi yake kwa nguvu.
5 Kuna mtu ambaye akinyamaza anaonekana ana hekima; hali mwingine huchukiwa kwa kuwa ni domo kaya mno.
6 Mtu mwingine hunyamaza kwani hana la kusema; na mwingine hunyamaza kwani anajua wakati wa kuongea.
7 Mwenye hekima atanyamaza mpaka wakati ufaao; Lakini domo kaya na mjinga huukosa wakati wa kufaa.
8 Mtu wa maneno mengi mno, atachukiwa, kadhalika na asiyewapa wengine nafasi ya kuongea.
9 Mtu aweza kupata bahati njema katika taabu; na bahati njema yaweza ikaishia katika hasara.
10 Kuna zawadi isiyokuletea faida yoyote; lakini zawadi nyingine huleta faida maradufu.
11 Mara nyingine fahari huleta hasara. Lakini wako wengine waliofaulu sana kutoka hali duni.
12 Mtu hununua vitu vingi kwa bei ya chini, kumbe hulipa mara saba zaidi ya bei yake.
13 Mwenye hekima hufanya apendeke kwa maneno yake; lakini uungwana wa wajinga ni bure tu.
14 Zawadi ya mpumbavu, haitakufaa kitu, maana anatazamia mengi kutoka kwako, si moja.
15 Yeye hutoa kidogo na kupiga domo sana, hufungua mdomo na kutangaza. Leo hukopesha, kesho anakitaka. Mtu kama huyo ni wa kuchukiza.
16 Mpumbavu husema, “Sina rafiki. Hakuna anayenishukuru kwa wema wangu. Wanakula chakula changu na kunisema vibaya.”
17 Naam! Ataendelea kuchekwa na wengi!

Mazungumzo yasiyofaa
18 Afadhali kuteleza sakafuni kuliko kuteleza kwa ulimi; maangamizi ya waovu yatakuja haraka.
19 Mtu asiye na shukrani ni kama hadithi isiyo wakati wake, na ambayo wajinga huirudiarudia.
20 Methali ikitoka kwa mpumbavu hukataliwa, maana haisemi wakati ulio wake.
21 Mtu aweza kuzuiwa kutenda dhambi kwa umaskini wake, kwa hiyo anapopumzika hatakuwa na la kujuta.
22 Mtu aweza kupoteza maisha yake kwa kuona aibu, au akayapoteza kuwaogopa watu.
23 Mtu aweza kumwahidi rafiki kitu kwa aibu, hata akamfanya kuwa adui bila sababu.
24 Uongo ni doa baya sana kwa mtu; uko daima mdomoni mwa mpumbavu.
25 Afadhali mwizi kuliko mwenye tabia ya uongo; lakini wote wawili wataangamia.
26 Tabia ya kusema uongo huleta fedheha, nayo itabaki daima na mwenye kusema uongo.
27 Anayaongea kwa hekima, ataendelea vizuri; mwenye busara atawapendeza wakuu.
28 Anayelima ardhi atapata mavuno kwa wingi; na anayewapendeza wakuu atajipatia haki.
29 Bakshishi na zawadi hupofusha macho ya wenye hekima, ni kizibo mdomoni cha kuwazuia wasikaripie ubaya.
30 Hekima ya kuficha na hazina iliyofichika, je, vina faida yoyote ile?
31 Afadhali mtu afichaye upumbavu wake, kuliko mtu afichaye hekima yake.

Generic placeholder image