6

1 Maana sifa mbaya huleta aibu na makaripio, kama yampatayo mwenye dhambi mdanganyifu.
2 Usikubali kutawaliwa na tamaa yako, la sivyo, itakuchana kama fahali,
3 itayakwanyua matawi yako ukapoteza matunda yako, ukaachwa kama mti ulionyauka.
4 Tamaa mbaya humwangamiza mwenyewe, na kumfanya awe kichekesho kwa maadui zake.

Urafiki
5 Maneno ya upole humwongezea mtu marafiki kuongea kwa adabu husababisha hisani.
6 Uwe na marafiki wengi wa kukusalimu, lakini wa kukushauri awe mmoja tu kati ya elfu.
7 Ukitaka kupata rafiki mpime kwanza, usiharakishe kumwamini.
8 Maana kuna rafiki aliye rafiki inapomfaa; siku ya taabu hatakuwako kukutegemeza.
9 Pia kuna rafiki abadilikaye kuwa adui, atazusha ugomvi ili kukuaibisha.
10 Pia yuko rafiki ambaye ni rafiki wakati wa mlo; lakini siku ya taabu hatakuwako kukutegemeza.
11 Ukipata fanaka atajifanya sawa nawe, na kuwaamuru watumishi wako.
12 Lakini ukifilisika atakugeuka; na kujificha mbali nawe.
13 Kaa mbali na maadui zako, na ujihadhari na rafiki zako.
14 Rafiki mwaminifu ni kinga imara; ampataye rafiki kama huyo amepata hazina.
15 Rafiki mwaminifu ana thamani kuliko chochote, hakuna awezaye kupima ubora wake.
16 Rafiki mwaminifu ni dawa itiayo nguvu mwilini, watu wamchao Bwana ndio wanaompata rafiki huyo.
17 Amchaye Bwana hupata marafiki wa kweli maana alivyo mtu ndivyo na rafiki zake.
18 Mwanangu, tangu ujana wako, chagua funzo, na hata uwapo mzee utaendelea kumpata Hekima.
19 Fanya bidii kama mkulima na mpanzi kumtafuta Hekima, na kungojea mavuno yake bora. Itakubidi kushughulika juu yake kwa muda, lakini muda si muda utakula mazao yake.
20 Watu wasio na nidhamu humwona Hekima kuwa mkali, wapumbavu hawakai naye kwa muda mrefu.
21 Kwao Hekima ni mzito kama jiwe la kupimia, nao hawakawii kumtupilia mbali.
22 Hekima kama jina lake lilivyo hajijulishi kwa watu wengi.
23 Mwanangu, nisikilize na kufuata shauri langu. Usikatae mawaidha yangu.
24 Tia pingu za Hekima miguuni mwako, na ukosi wake shingoni mwako.
25 Beba mzigo wake, wala usichoke na vifungo vyake.
26 Mwendee kwa roho yako yote, na kushika njia zake kwa nguvu zako zote.
27 Mchunguze na kumtafuta, naye atajijulisha kwako. Ukisha mpata usimwachilie.
28 Mwishowe utapata pumziko kwake, naye atakuwa ndiye furaha yako.
29 Pingu zake zitakuwa ngome yako imara, na ukosi wake utakuwa ushanga wa thamani.
30 Nira yake ni pambo la dhahabu na vifungo vyake ni mkufu wa buluu.
31 Hekima atakuwa kwako kama vazi la heshima, atakuwa kama taji la furaha kichwani pako.
32 Mwanangu, ukitaka, utafundishwa; pania kujifunza nawe utakuwa na akili.
33 Ukipenda kusikiliza, utapata maarifa; ukitega sikio lako, utakuwa mwenye hekima.
34 Ukienda kwenye mkutano wa wazee, akiwako mzee mwenye hekima ambatana naye.
35 Uwe tayari kusikiliza kila fundisho, na usiziache methali za hekima kukuponyoka.
36 Ukimwona mwenye hekima, mwendee mapema, kichakaze kizingiti cha nyumba yake kwa kumtembelea.
37 Zitafakari kanuni za Bwana, jishughulishe na amri zake. Yeye ataiimarisha akili yako, na hekima unayotamani utajaliwa.

Generic placeholder image