7

Mawaidha mengine
1 Usifanye uovu, na uovu wowote hautakupata.
2 Epa ubaya, nao utakukimbia.
3 Mwanangu, usilime ardhi kupanda udhalimu, la sivyo utavuna udhalimu mara saba.
4 Usiombe cheo kikubwa kwa Bwana, wala kiti cha heshima kwa mfalme.
5 Usijioneshe kuwa mwadilifu mbele ya Bwana, wala usioneshe hekima yako mbele ya mfalme.
6 Usijaribu kutafuta kuwa hakimu, usije ukashindwa kutokomeza uovu; usije ukapotoshwa na mwenye nguvu, na hivyo kusababisha kupoteza unyofu wako.
7 Usiiudhi jumuiya ya wananchi, wala usijivunjie heshima miongoni mwa watu.
8 Usivutwe kutenda dhambi mara mbili, maana hutaacha kuadhibiwa hata kwa mmoja.
9 Usiseme, “Mungu atapokea wingi wa sadaka zangu; nikimtolea Mungu Mkuu tambiko lazima atapokea.”
10 Usisitesite katika sala, wala usisahau kuwapa maskini sadaka.
11 Usimcheke aliye na huzuni rohoni, maana Mungu anayemnyenyekeza mtu aweza pia kumwinua.
12 Usitunge uongo dhidi ya ndugu yako, wala usimtendee hivyo rafiki yako.
13 Kataa kabisa kusema uongo, maana uongo hauleti jema lolote.
14 Usipayukepayuke kwenye mkutano wa wazee, wala kujirudiarudia katika sala zako.
15 Usichukie kazi ngumu, au kazi ya shambani iliyopangwa na Mungu Mkuu.
16 Usijiunge na genge la wenye dhambi, kumbuka kuwa adhabu haitakawia.
17 Uwe mnyenyekevu kabisa, maana adhabu ya wasiomcha Mungu ni moto na mabuu.

Uhusiano na wengine
18 Usimsaliti rafiki ili kujipatia fedha, au rafiki wa kweli kujipatia dhahabu ya Ofiri.
19 Uoe mwanamke mwenye hekima na mwema; mwanamke mwema ni bora kuliko dhahabu.
20 Usimtendee vibaya mtumishi mwaminifu kazini, au kibarua aliyejitolea kukutumikia vema.
21 Mpende mtumwa mwenye akili kwa moyo wote; usimnyime mtumwa wa namna hiyo uhuru wake.
22 Je, una mifugo? Basi, ichunge! Kama ina faida kwako, baki nayo.
23 Je, una watoto? Basi, wafunze nidhamu. Wafundishe utii tangu utoto wao.
24 Je, una watoto wa kike? Wafunze usafi wa mwili, lakini usiwabembeleze mno.
25 Ukimwoza binti yako utakuwa umetimiza kazi kubwa. Lakini mwoze kwa mwanamume mwenye busara.
26 Unaye mke anayekupendeza? Usimpe talaka. Lakini kama humpendi, usimwamini.
27 Mheshimu baba yako kwa moyo wako wote, wala usisahau uchungu wa mama yako alipokuzaa.
28 Kumbuka kwamba wao ndio waliokuzaa. Je, unaweza kuwalipa yote waliyokutendea?
29 Mche Bwana kwa moyo wako wote; na wape heshima makuhani wake.
30 Mpende Muumba wako kwa nguvu zako zote, na usiwatupe wahudumu wake.
31 Mche Bwana na kuwaheshimu makuhani. Mpe Bwana sehemu ulivyoamriwa: Mazao ya kwanza, tambiko ya hatia, kidari, na zaka zote zinazotakiwa.
32 Wape maskini kwa ukarimu, ili Bwana akupe baraka zake kikamilifu.
33 Ukarimu wako uwe kwa watu wote, wala usiwanyime ukarimu hata marehemu.
34 Usiwape kisogo wanaoomboleza, bali ushiriki huzuni ya walio na huzuni.
35 Usiache kuwatembelea wagonjwa; maana ukiwatembelea utapendwa.
36 Katika matendo yako yote kumbuka mwisho wako, nawe hutatenda dhambi kamwe.

Generic placeholder image