47

Nathani
1 Baada yake alitokea Nathani; yeye alikuwa nabii siku za Daudi.

Daudi
2 Kama vile mafuta ya tambiko ya amani yanavyochaguliwa na kutengwa kwa ajili ya Bwana, ndivyo na Daudi alivyoteuliwa miongoni mwa watu wa Israeli.
3 Alicheza na simba kana kwamba ni wanambuzi na dubu kana kwamba ni wanakondoo.
4 Wakati wa ujana wake aliliua jitu, akawaondolea watu wake matukano yake. Alirusha jiwe kwa kombeo lake, likamwangusha Goliathi, mwenye majivuno.
5 Maana alimsihi Bwana, Mungu Mkuu naye akauimarisha mkono wake wa kulia, apate kumuua adui mwenye nguvu vitani, na kukuza nguvu za watu wake.
6 Watu walimsifu kwa kuua maadui 10,000, na kumshangilia kwa baraka za Bwana wakati alipovikwa taji la kifalme.
7 Aliwafagilia mbali maadui zake pande zote, na kuwatokomeza kabisa Wafilisti; alizivunjavunja nguvu zao mpaka leo.
8 Katika yote aliyoyatenda Daudi, alimshukuru na kumtukuza yule Mtakatifu Mungu Mkuu. Alimpenda Muumba wake na kumwimbia sifa kwa moyo wake wote.
9 Aliwaweka waimbaji mbele ya madhabahu, ili kwa sauti zao waimbe nyimbo tamu.
10 Sikukuu alizifanya ziwe nzuri, na kuzipangia nyakati zake mwaka mzima, wakati watu waliposifu jina takatifu la Mungu, na hekalu kujaa nyimbo nzuri tangu asubuhi.
11 Bwana alimwondolea Daudi dhambi zake, na kuikuza nguvu yake milele; alimjalia haki ya kuwa mfalme, akaweka kiti cha enzi kitukufu katika Israeli.

Solomoni
12 Baada ya Daudi alifuata mwanawe mwenye hekima ambaye aliishi kwa amani kwa sababu yake.
13 Solomoni alitawala wakati wa amani. Mungu alimjalia amani pande zote, ajenge nyumba kwa heshima ya jina lake, na kutayarisha hekalu la kudumu milele.
14 Kweli ulikuwa na hekima ewe Solomoni ulipokuwa kijana! Ulitiririka busara kama mto!
15 Ulijulikana duniani kwa maarifa yako, na kuijaza methali na vitendawili.
16 Jina lako lilijulikana mpaka visiwa vya mbali, watu wakakupenda kwa kuwaletea amani.
17 Kwa nyimbo, methali, mifano na maelezo yake, nchi zilishikwa na mshangao.
18 Kwa heshima ya jina la Bwana Mungu ambaye anaitwa Mungu wa Israeli, ulikusanya dhahabu kama bati, na fedha kama madini ya risasi.
19 Lakini ukautoa mwili wako kwa wanawake, ukawa mtumwa wa tamaa zako.
20 Uliitia doa heshima yako, na kuutia unajisi ukoo wako, hata ukawaletea wazawa wako adhabu, wakahuzunishwa kwa sababu ya upumbavu wako.
21 Hata ufalme ukagawanyika sehemu mbili, ufalme pinzani ukatokea huko Efraimu.
22 Lakini Bwana hataacha kuwa na huruma, wala kuruhusu kazi yake yoyote iharibike; hatawafutilia mbali wazawa wa Daudi, mteule wake, wala kuangamiza ukoo wa huyo aliyempenda. Kwa hiyo alimwachia Yakobo mabaki, na Daudi mzizi wa jamaa yake.

Rehoboamu na Yeroboamu
23 Solomoni akafariki kama wazee wake, akamwacha mmoja wa watoto wake kuwa mtawala. Huyo alikuwa Rehoboamu, mwingi wa upumbavu na mtovu wa busara, ambaye maongozi yake yaliwafanya watu wakaasi. Kulikuwa pia na Yeroboamu mwana wa Nebati, aliyewasababisha Waisraeli kutenda dhambi, na kuwaongoza Waefraimu katika njia ya dhambi.
24 Dhambi zao zilizidi kuwa nyingi mno, hata zikasababisha waondolewe nchini mwao.
25 Maana walijaribu kutenda kila aina ya uovu, mpaka Bwana alipowalipiza kisasi.

Generic placeholder image