30

Malezi
1 Mzazi ampendaye mwanawe, atamrudi mara kwa mara, ili amwonee fahari jinsi atakavyokua.
2 Amfunzaye mwanawe nidhamu, baadaye atafaidika naye. Atajivunia mwanawe mbele ya wanaofahamiana naye.
3 Anayemfundisha mwanawe atawafanya maadui zake waone wivu, na kujivunia mwanawe mbele ya rafiki zake.
4 Hata kama baba yake amekufa atakuwa kama hakufa, maana ameacha nyuma mtoto anayefanana naye.
5 Baba alipokuwa hai alifurahi kuwa pamoja naye, na akifa hana haja ya kusikitika.
6 Baba amemwacha nyuma atakayelipiza kisasi maadui zake, na atakayelipa wema wa rafiki zake.
7 Anayemharibu mwanawe, atakuwa na kazi ya kufunga vidonda, na kwa kila kilio moyo wake utashtuka.
8 Farasi aliyezoezwa vibaya atakuwa mkaidi, na mtoto asiyefunzwa nidhamu atageuka kuwa mkaidi.
9 Mbembeleze sana mtoto naye atakutisha, chezacheza naye, naye atakusikitisha.
10 Usichekecheke naye kama hupendi kulia naye baadaye; matokeo yake mwishoni itakuwa kusaga meno.
11 Usimruhusu kufanya apendavyo alipo bado mtoto, na wala usiache kumkosoa anapokosa.
12 Mfanye awe na utii angali bado mtoto, mtandike wakati alipo bado kijana; la sivyo, atakuwa mkaidi na kuacha kukutii, na kukuhuzunisha mno rohoni.
13 Mfunze mwanao nidhamu na kuwa mvumilivu, ili usije ukaaibishwa na aibu yake.

Afya
14 Afadhali maskini mwenye afya na nguvu mwilini, kuliko tajiri anayeteseka mwilini mwake.
15 Afya na nguvu ni bora kuliko dhahabu; mwili wenye nguvu ni bora kuliko utajiri mwingi.
16 Hakuna utajiri ulio bora kuliko afya ya mwili, na hakuna furaha iliyo bora kuliko furaha ya moyoni.
17 Afadhali kifo kuliko maisha ya taabu, na pumziko la milele kuliko ugonjwa wa kudumu.
18 Kumpa chakula bora mtu asiyeweza kula ni kama kuweka chakula juu ya kaburi:
19 Je, sadaka yafaa nini kwa sanamu ambayo haiwezi kula wala kunusa? Hivyo ndivyo alivyo mtu anayeteswa na Bwana.
20 Mtu huyo huona kwa macho yake na kuguna, kama towashi anayemkumbatia msichana na kuguna.

Furaha na huzuni
21 Usijiachilie kupata huzuni, wala usijiumize mwenyewe kwa makusudi.
22 Furaha ya moyo ni uhai wa mtu; furaha ndiyo inayompa maisha marefu.
23 Jifurahishe na kuwa na utulivu wa moyo; weka huzuni mbali nawe. Maana huzuni imewaangamiza wengi, wala haina faida kwa mtu yeyote.
24 Wivu na hasira hufupisha maisha, mahangaiko humfanya mtu azeeke upesi.
25 Mwenye moyo mkunjufu na mwema, atachukua hadhari juu ya chakula anachokula.

Generic placeholder image