36

Sala kwa ajili ya Israeli
1 Utuhurumie ee Bwana Mungu wa wote; Yafanye mataifa yote yakuogope. Inua mkono wako dhidi ya mataifa mengine,
2 uyafanye yauone uwezo wako mkuu.
3 Kama ulivyotutumia kuyaonesha jinsi ulivyo mtakatifu, vivyo hivyo yatumie kutuonesha utukufu wako.
4 Nayo yatajua kama tunavyojua na sisi, kwamba hakuna Mungu ila wewe, ee Bwana.
5 Fanya tena ishara na kufanya miujiza zaidi, ufanye mkono wako uwe na utukufu zaidi.
6 Onesha hasira yako na kumwaga ghadhabu yako; waangamize wapinzani na kuwafuta maadui.
7 Iharakishe ile siku na kukumbuka kiapo chako;
8 wafanye watu wasimulie matendo yako makuu. Yeyote atakayeponyoka ateketezwe na ghadhabu yako kali, na wale wanaowadhuru watu wako wapate maangamizi.
9 Uwaponde wakuu wa maadui zako, ambao husema: “Hakuna mwingine ila sisi wenyewe!”
10 Yakusanye pamoja makabila yote ya Yakobo, uwape mali yako kama ulivyopanga mwanzoni.
11 Wahurumie ee Bwana watu wanaoitwa kwa jina lako; Waisraeli uliowaita mzaliwa wako wa kwanza wa kiume.
12 Uuonee huruma mji wa hekalu lako, Yerusalemu, mji wa pumziko lako.
13 Uujaze mji wa Siyoni shangwe za matendo yako ya ajabu, na hekalu lako lijae utukufu wako.
14 Uwahakiki watu wako uliowaumba mwanzoni, na kutimiza unabii uliosemwa kwa jina lako.
15 Uwatuze wale wanaokungojea, na manabii wako waonekane kuwa ni wa kuaminika.
16 Usikilize, ee Bwana, sala ya watumishi wako, kulingana na baraka za Aroni juu ya watu wako.
17 Hivyo binadamu wote duniani watajua kuwa wewe ndiwe Bwana, Mungu wa nyakati zote.

Kuchagua mke
18 Chakula chochote chaweza kuliwa, lakini chakula kingine ni bora kuliko kingine.
19 Kama ulimi upimavyo mionjo ya aina ya vyakula, ndivyo na mwenye akili agunduavyo maneno ya uongo.
20 Mwenye akili potovu atasababisha huzuni, lakini mwenye uzoefu wa maisha atamlipa inavyofaa.
21 Mwanamke aweza kuolewa na yeyote, akini msichana mmoja ni bora kuliko mwingine.
22 Uzuri wa mwanamke hufurahisha uso, na hushinda kila kitu anachotamani mwanamume.
23 Kama mwanamke ni mwema na mwenye adabu anapoongea, mumewe ana bahati kuliko wengine wote.
24 Mwanamume akipata mke amepata ubora mkubwa mno, amejipatia msaidizi bora na nguzo ya msaada.
25 Mali isiyolindwa kwa ukuta itaporwa; ni pasipo mke, mwanamume atatangatanga na kusononeka.
26 Nani atakayemwamini jambazi azururaye mji hata mji?
27 Hivyo hakuna atakayemwamini mwanamume asiye na kwake, ambaye ana malazi popote usiku unapomkuta.

Generic placeholder image