19

Wamisri na Waisraeli kwenye Bahari ya Shamu
1 Hasira yako isiyo na upeo iliwajia wale waovu bila huruma. Wewe ulijua kabla mambo yale ambayo walikuwa wanataka kuyafanya.
2 Ulijua kwamba baada ya kuwaachilia watu wako waondoke, na hata baada ya kuwaharakisha waende zao, watabadili nia yao na kuwafuatia.
3 Kweli, ingawa walikuwa bado wanaomboleza na kufanya matanga kwenye makaburi ya watu wao waliokufa, waliamua jambo jingine la kipumbavu kabisa; waliwafuatia hao ambao awali waliwasihi na kuwashawishi waondoke.
4 Naam, balaa walilostahili liliwaongoza hata mwisho huo, likawafanya wasahau mambo yaliyowapata; ili juu ya mateso yao waongeze adhabu iliyokosekana.
5 Na watu wako wakiwa katika safari yao ya ajabu, hao maadui walikuwa wakivamiwa na kifo cha kutisha.

Mungu awalinda watu wake
6 Maumbile yote yalirekebishwa, kulingana na amri zako, kusudi watu wako wasipate madhara.
7 Mbingu ziliweka kivuli juu ya kambi yao, na nchi kavu ikatokea pale palipokuwa na maji, uwanja wenye majani ulitokea katika mawimbi ya bahari, pakawa na barabara ya kupitia bila pingamizi.
8 Watu wako wote wakavuka, baada ya kuona muujiza huo, wakilindwa kwa mkono wako.
9 Walizungukazunguka kama farasi wakarukaruka kama wanakondoo wakikutukuza wewe, ee Bwana, uliyewaokoa.
10 Wakati huo walikumbuka bado yaliyotukia walipokuwa ugenini: Nchi ilijaa viroboto kwa wingi badala ya ng'ombe, mto ukajaa vyura badala ya samaki.
11 Baadaye waliona namna ya ndege wapya,
12 walipotamani vyakula vitamu zaidi, wakapewa kware kutoka baharini, kuwashibisha.

Adhabu ya Wamisri
13 Lakini wale watu waovu walipata adhabu, baada ya kuonywa kwa nguvu za ngurumo; walipata mateso waliyostahili kwa ubaya wao. Hakuna taifa lililowachukia wageni kama taifa hilo;
14 wapo watu wengine waliokataa kupokea wageni waliowatembelea, lakini watu hawa waliwafanya wageni wao kuwa watumwa; wageni ambao hapo mwanzo walikuwa wema kwao.
15 Afadhali wale waliokataa kupokea wageni, ingawa nao watapata adhabu yao;
16 lakini watu hawa Wamisri kwanza waliwapokea kwa shangwe na kuwatendea kama raia, kisha baadaye wakawafanya wateseke kikatili kabisa.
17 Watu hawa nao walivamiwa na upofu kama wale watu wa Sodoma mlangoni mwa yule mtu mwadilifu. Walivamiwa na giza tupu, kila mtu akatafuta njia katika mlango wake mwenyewe.

Nguvu kuu ya Mungu
18 Kinubi kina nyuzi kadha wa kadha na kila uzi una sauti yake, lakini kila sauti yaweza kuwekwa pamoja na nyingine ukapata sauti tofauti. Hivyo ndivyo ilivyokuwa siku zile wakati maumbile yenyewe yalipoingia kwenye mchanganyiko mpya. Tazama ilivyotukia:
19 Viumbe vya nchi kavu viligeuka kuwa viumbe vya majini, vile vya majini vikatembea juu ya nchi kavu;
20 moto ulizidi kuwaka katika mvua, maji yakasahau asili yake - kuzima moto!
21 Hata hivyo, moto huo haukuweza kuunguza wale wanyama waangamiao waliokuwa wakitembea katikati yake, wala haukuweza kuyeyusha kile chakula cha mbinguni ambacho kilifanana na theluji na kiliyeyuka kwa urahisi.

Hatima
22 Naam, wewe ee Bwana wawakuza na kuwatukuza watu wako kwa kila namna, wala hukuacha kuwasaidia nyakati zote na mahali popote!

Generic placeholder image