3

1 Lakini watu wanyofu wako mikononi mwa Mungu, Mateso yoyote hayatawapata kamwe.
2 Kwa wapumbavu walionekana kwamba wamekufa na kwamba kufariki kwao kulikuwa jambo baya;
3 kuondoka kwao kwetu kulidhaniwa kuwa uharibifu, lakini ukweli ni kwamba wamo katika amani.
4 Waonavyo watu ni kwamba wameadhibiwa, lakini wanalo tumaini thabiti la kutokufa.
5 Waliadhibiwa kidogo tu, lakini sasa watapokea tuzo kubwa; Mungu aliwajaribu akawapata wanastahili kuishi kwake.
6 Aliwajaribu kama dhahabu katika tanuri, akawapokea kama tambiko ya kuteketezwa.
7 Wakati wa kupata tuzo utakapofika, watangaa, watameremeta kama vimulimuli katika nyasi kavu.
8 Watayahukumu na kuyatawala makabila na mataifa, naye Bwana atatawala juu yao milele.
9 Wote wamwaminio Mungu watatambua ukweli wake; wote walio waaminifu watakaa kwake kwa upendo, maana huwajalia neema na huruma watakatifu wake, na huwaangalia kwa wema hao aliowateua.
10 Lakini wabaya wataadhibiwa kadiri ya fikira zao mbovu, naam, wasiojali mambo ya uadilifu, wote waliomwasi Bwana.
11 Wote wanaodharau hekima au nidhamu wana bahati mbaya; tumaini lao ni bure, jasho lao haliwafaidii chochote; na matendo yao ni ya bure.
12 Wake zao huwa wapumbavu na watoto wao wapotovu; wazawa wao watakuwa katika laana.

Umuhimu wa fadhila
13 Heri mwanamke tasa ambaye hana hatia ambaye hajahusika na muungano ulio dhambi; huyo atapata tuzo Mungu atakapohukumu roho za watu.
14 Heri pia towashi asiyevunja sheria kwa mikono yake, ambaye hajafikiria maovu dhidi ya Bwana; huyo atapata upendeleo maalumu kwa uaminifu wake, na mahali pa furaha kuu katika hekalu la Bwana.
15 Maana matunda ya kazi njema ni utukufu; ni kama mizizi welekevu inayochipua daima.
16 Lakini watoto wa wazinzi watakufa kabla ya kukomaa; naam, wazawa wa wazinzi wataangamia.
17 Na hata wakiishi sana hakuna atakayewajali, na hatimaye uzee wao hautakuwa na heshima.
18 Wakifa vijana hawatakuwa na tumaini, wala hawatapata kitulizo wakati wa hukumu.
19 Maana mwisho wa watu wasio waadilifu ni balaa tupu.

Generic placeholder image