9

Sala ya kuomba Hekima
1 “Ee Mungu wa wazee wetu, Bwana mwenye huruma! Kwa neno lako uliumba vitu vyote.
2 Kwa Hekima yako ulimuumba mtu avitawale viumbe ulivyoumba,
3 aumiliki ulimwengu kwa utakatifu na uadilifu, na kutekeleza haki kwa moyo mnyofu.
4 Nakuomba unipe Hekima anayekaa kando ya kiti chako cha enzi; wala usinikatae mimi miongoni mwa watumishi wako.
5 Mimi ni mtumishi wako, mtoto wa mjakazi wako, mtu dhaifu asiye wa siku nyingi, wala sina nguvu ya kuelewa hukumu na sheria.
6 Hata kama mtu yeyote akiwa mkamilifu kiasi gani, bila Hekima atokaye kwako atakuwa bure tu.
7 Ulinichagua mimi kuwa mfalme wa watu wako, hakimu wa wanao wa kiume na wa kike.
8 Uliniagiza nijenge hekalu juu ya mlima wako mtakatifu, na madhabahu katika mji uliochagua kuwa makao yako, mfano wa hema takatifu uliyoifanya tangu awali.
9 Hekima yupo pamoja nawe; naye ajua matendo yako; alikuwa pamoja nawe wakati ulipoumba ulimwengu. Hekima anajua yanayokupendeza, na yaliyo sawa kulingana na amri zako.
10 Umpeleke, basi, kutoka mbingu tukufu, kutoka kiti chako cha enzi kitukufu, ili akae nami na kufanya kazi pamoja nami, nipate kujifunza yale yanayokupendeza.
11 Maana Hekima anajua na anaelewa mambo yote, naye ataniongoza kwa busara katika matendo yangu; kwa utukufu wake atanilinda.
12 Hapo matendo yangu yatakubalika. Nitawahukumu watu wako kwa haki na kustahili kuwa katika kiti cha enzi cha baba yangu.
13 “Nani awezaye kuijua nia ya Mungu? Au nani awezaye kufahamu matakwa yake?
14 Akili ya binadamu haifai kitu na elimu yetu huelekea kupotosha,
15 kwa maana miili yetu yenye kufa hugandamiza roho zetu. Mwili uliotengenezwa kwa udongo, ni mzigo kwa akili timamu.
16 Twabahatisha tu kupambanua juu ya mambo ya duniani; na yale yaliyo karibu nasi ni jasho kuyafahamu. Nani basi, atakayefaulu kujifunza yaliyoko mbinguni?
17 Hakuna aliyeweza kujifunza mashauri yako, ee Mungu, isipokuwa kwanza umempa Hekima na kumpelekea roho yako kutoka juu.
18 Ndivyo njia za watu duniani zilivyowekwa sawa, wakajifunza yanayokupendeza na kuokolewa na Hekima.”

Generic placeholder image