4

1 Afadhali kukosa watoto na kuwa mnyofu, maana unyofu wako utakumbukwa milele, na unatambuliwa na Mungu na wanaadamu.
2 Unyofu wako utawapa watu fursa ya kuuiga, na usipokuwapo watu watasikitika kuukosa. Siku zote unapita umevikwa taji ya ushindi, mshindi katika mashindano ya tuzo zisizo na dosari.
3 Lakini wazawa wengi wa wasiomcha Mungu hawafai kitu, watoto wao haramu hawawezi kutoa mizizi wala kuwa na msingi imara.
4 Na hata wakitoa matawi ni ya muda tu, bila mizizi imara watatikiswa na upepo na kwa nguvu za dhoruba watangolewa.
5 Matawi yao yatavunjika kabla ya kukomaa, matunda yao hayatafaa chochote, hayataiva yaliwe, ni bure kabisa.
6 Watoto waliozaliwa haramu watashuhudia juu ya uovu wa wazazi wao wakati wa hukumu.
7 Lakini mtu mwema, hata akifa kijana, atapata pumziko.
8 Uzee unaheshimika sio tu kwa urefu wa maisha, wala haupimwi kwa wingi wa miaka.
9 Hekima na maisha mema ni ishara ya kukomaa; hivyo huja pamoja na uzee.
10 Palikuwa na mtu aliyempendeza Mungu naye Mungu akampenda, wakati alipokuwa anaishi kati ya wenye dhambi, Mungu alimchukua,
11 akamhamisha ili uovu usibadili busara yake udanganyifu usiweze kuipotosha roho yake.
12 Mvuto wa uovu huzuia wema usionekane; hata mtu asiweze kuona jambo jema mbele yake; upepo wa tamaa waweza kumpotosha mtu mnyofu.
13 Huyo alifikia ukamilifu kwa muda mfupi tu, akawa ametimiza miaka mingi.
14 Maisha yake yalimpendeza Bwana, naye akaharakisha kumtoa kati ya uovu. Watu waliona jambo hilo lakini hawakuelewa; hawakuweza kutambua jambo hili moja:
15 Kwamba Mungu ni mwema na mwenye huruma kwa watu wake; huwalinda hao aliowateua kuwa wake.
16 Mtu mwema ambaye amekwisha kufa atawahukumu wasiomcha Mungu walio hai. Kijana aliyefikia hali ya ukamilifu upesi, atamwaibisha mzee mkongwe aliye dhalimu.
17 Watu waovu watamwona mwenye busara anakufa lakini hawataelewa matakwa ya Bwana juu yake, wala kwa sababu gani alimweka salama.
18 Watadhihaki kifo cha mtu mwema lakini Bwana atawacheka. Wao watakapokufa hawatazikwa kwa heshima; na hata wafu watawapuuza milele.
19 Bwana atawatupa chini na kuwanyamazisha; atawatikisa mpaka misingi yao, watakuwa magofu matupu na ukiwa wataaibika kwa uchungu. Hakuna mtu atakayewakumbuka tena.

Tofauti ya wema na waovu wakati wa hukumu
20 Waovu wataingia hukumuni kwa hofu na woga dhambi zao zitakapohesabiwa, matendo yao maovu yatawahukumu mbele ya macho yao.

Generic placeholder image