2

1 Katika upotovu wao huambiana: “Maisha yetu ni mafupi na yenye taabu. Kifo kinapowasili hakuna dawa ya kuepukana nacho. Hakuna mtu aliyewahi kumtoa mwingine ahera.
2 Sisi tulizaliwa kwa bahati tu, tukisha kufa itakuwa kana kwamba hatukupata kuwapo. Pumzi yetu ni kama moshi tu unaotoweka; akili zetu ni ndogo tu zinazowashwa kwa mapigo ya mioyo yetu.
3 Cheche hiyo ikizimika, mwili wetu utageuka majivu, na roho yetu itatoweka kama vile hewa.
4 Jina letu litasahaulika punde si punde, mambo tuliyotenda hayatakumbukwa; maisha yetu yatatoweka kama nyayo za mawingu; yatatawanywa kama ukungu unaofukuzwa na nuru ya jua, unaoshindwa kustahimili joto la jua.
5 Siku zetu ni kama kivuli kipitacho, na tukisha kufa hatuwezi kurudi kutoka humo. Siku ya kufa imepangwa wala hakuna atakayeweza kuirudisha.
6 Hivyo na tujifurahishe kwa chochote kizuri kilichopo; tuvitumie kabisa viumbe kama wakati wa ujana.
7 Tujishibishe divai ya thamani na marashi, tujichumie maua ya vuli yasitupite.
8 Tujivike taji za waridi kabla hayajanyauka.
9 Kila mmoja wetu ashiriki tamasha zetu, tuache alama za anasa zetu zionekane kila mahali. Maana ndivyo maisha yalivyo! Ndiyo tuliyopangiwa.
10 “Maskini, hata akiwa mwema, tutamkandamiza; naye mjane hatutamhurumia wala kumjali mzee mwenye mvi.
11 Nguvu zetu ndizo mwongozo wa haki, mnyonge hana faida yeyote!
12 Tena, tumvizie mtu mwema; mtu huyo ni usumbufu kwetu na hutupinga. Hutukaripia kila tunapovunja sheria; hutushtaki kila tunapokiuka mwongozo.
13 Mtu mwema hujitakia kumjua Mungu na kujiita mtoto wake Bwana.
14 Mtu wa namna hiyo amekuwa kwetu karipio la fikira zetu.
15 Hata tu kumtazama ni mzigo kwetu; maana anaishi tofauti na watu wengine njia zake ni ngeni kabisa.
16 Anatuona sisi kuwa kama madini hafifu; huziepa njia zetu kama kukwepa uchafu. Huuthamini kuwa heri mwisho wa mwadilifu, na hujigamba kwamba Mungu ni Baba yake.
17 Haya, na tuone kama maneno yake ni ya kweli! Tuone yatakayompata wakati atakapokufa.
18 Kama kweli yeye ni mwana wa Mungu, Mungu atamsaidia, na kumkomboa makuchani mwa maadui zake.
19 Haya! Tumtendee kikatili na kumtesa, tuone alivyo mpole, tuujaribu uvumilivu wake.
20 Tutamhukumu kifo cha aibu maana, kama alivyosema, Mungu atamwokoa!”

Mambo ya nje hudanganya
21 Ndivyo wafikiriavyo waovu, lakini wanajidanganya wenyewe. Uovu wao umewapofusha.
22 Hawajui mipango ya siri ya Mungu; hawajawahi kutumaini kupata thawabu ya kuishi vema, wala kulitambua tuzo la watu waishio bila hatia.
23 Mungu aliumba watu waishi maisha ya milele aliwafanya kwa mfano wa hali yake mwenyewe.
24 Lakini kwa wivu wa Shetani kifo kiliingia duniani, na wote walio upande wake hukipata.

Generic placeholder image