10

1 Hekima alimlinda yule aliyeumbwa kwanza, baba wa ulimwengu, aliyeumbwa peke yake kabla ya wengine. Hekima alimwokoa kutoka kosa lake,
2 akampa nguvu ya kutawala vitu vyote.
3 Lakini mtu mmoja mkosefu alijitenga naye katika hasira yake, akaangamia kwa kumuua ndugu yake kutokana na ghadhabu yake.
4 Kwa sababu ya mtu huyo gharika ilifurika duniani, lakini kwa mara nyingine Hekima aliiokoa. Alimwongoza mtu mmoja mwadilifu juu ya gharika katika mtumbwi dhaifu.
5 Tena, mataifa yalipoafikiana katika uovu wao, Hekima alimtambua mtu mmoja mwadilifu, akanihifadhi katika unyofu wake mbele ya Mungu. Hekima alimpa mtu huyo moyo wa kufuata amri ya Mungu hata ingawa alimpenda sana mwanawe.
6 Wakati watu waovu walipokuwa wanaangamizwa, Hekima ndiye aliyemsalimisha mtu mmoja mwadilifu; alimwokoa katika moto ulioshuka mbinguni na kuteketeza Miji Mitano.
7 Hata sasa, ushahidi wa uovu wao unaonekana: Nchi ya mahala hapo ni kame na inafuka moshi; mimea ya hapo huzaa matunda lakini hayakomai kamwe; na jiwe la chumvi limesimama hapo, kumbukumbu la mtu asiyeamini.
8 Watu wa miji hiyo walimpuuza Hekima, wasiweze kubainisha kati ya jema na baya. Zaidi ya hayo, waliacha kumbukumbu la upumbavu wao, ili kushindwa kwao kusisahaulike kamwe.
9 Lakini Hekima aliwasalimisha hatarini wale waliomngojea kwa saburi.
10 Mtu mmoja mwadilifu alipoikimbia ghadhabu ya ndugu yake, Hekima alimwongoza katika njia sawa. Alimwonesha ufalme wa Mungu na kumjulisha mambo matakatifu. Hekima alimfanikisha katika kazi zake; alimzidishia mazao ya kazi zake.
11 Wadhalimu walipotaka kunyakua mali yake kwa wivu, Hekima alikaa upande wake na kumtajirisha.
12 Hekima alimlinda na maadui zake na kumwokoa na wale waliomvizia. Katika mapigano makali Hekima alimpa ushindi, apate kutambua kwamba wema una nguvu kupita chochote.
13 Tena mtu mmoja mwadilifu alipouzwa utumwani, Hekima hakumwacha, ila alimweka salama mbali na dhambi. Hekima aliandamana naye gerezani,
14 wala humo gerezani hakumwacha, mpaka alipompa madaraka juu ya ufalme na kumfanya mtawala juu ya mabwana zake. Wale waliomshtaki akawadhihirisha kuwa waongo, akamjalia heshima ya milele.

Kutoka Misri
15 Hekima aliwaokoa watu watakatifu wasio na hatia makuchani mwa taifa lililowadhulumu.
16 Aliingia ndani ya roho ya mtumishi mmoja wa Bwana, naye kwa maajabu na ishara akawapinga wafalme wenye kutisha.
17 Hekima aliwapa watu wa Mungu tuzo la jasho lao; aliwaongoza katika njia ya ajabu akawa kwao kivuli mchana na mwanga wa nyota usiku.
18 Hekima aliwavusha Bahari ya Shamu, akawaongoza katikati ya maji mengi,
19 lakini akawazamisha maadui zao akaitosa miili yao ufuoni kutoka vilindini.
20 Hivyo waadilifu wakawapokonya watu waovu, wakaimba kulisifu jina lako takatifu, ee Bwana, wote pamoja wakakutukuza kwa vile uliwapigania.
21 Hekima aliwafumbua bubu vinywa wakaongea, na kufanya ndimi za watoto wachanga kuongea waziwazi.

Generic placeholder image