13

Upumbavu wa kuabudu viumbe
1 Watu wote ambao hawajapata kumjua Mungu ni wapumbavu mpaka ndani. Watu hao wameviona vitu vizuri vilivyopo, lakini wameshindwa kumjua Mungu ambaye ndiye hasa, anayeishi. Hutazama hivyo viumbe, vilivyo kazi yake yeye, lakini hawamtambui yeye fundi aliyeviumba.
2 Badala yake, walidhani kwamba moto, upepo, dhoruba, vimondo, mafuriko ya maji ama viumbe vya angani, ndiyo miungu itawalayo ulimwengu.
3 Huenda watu walishangazwa kwa uzuri wa vitu hivyo, wakavidhani kuwa miungu, lakini wangalipaswa kutambua kwamba viumbe hivyo vina Mwenyewe, naye avipita hivyo vyote. Huyo ndiye chanzo cha uzuri na ndiye aliyeviumba hivyo.
4 Kwa vile watu wanashangazwa na uwezo na nguvu za viumbe hivyo, basi wanapaswa kujifunza kutokana na viumbe hivyo kwamba huyo aliyeviumba ana nguvu zaidi.
5 Kadiri uzuri wa viumbe ulivyo mkubwa, kadiri hiyohiyo binadamu awezavyo kujifunza juu ya Muumba wake.
6 Lakini, labda watu hao hawana hatia sana. Huenda ikawa walikosea tu, walipokuwa wanamtafuta Mungu kweli na kutamani kumwona.
7 Wakiwa wamezungukwa na viumbe vya Mungu, huvichunguza kwa makini hata mwishowe huviona hivyo vitu kuwa vizuri kweli na kuviamini.
8 Lakini hata hivyo, hawawezi kujitetea kwamba hawana hatia.
9 Maana, ikiwa wanao uwezo wa kujua hayo yote, hata waweze kuuchunguza ulimwengu, walishindwaje kumjua yeye aliye Bwana wa vitu vyote hivi?
10 Lakini walio duni kupita wote ni watu wale wanaotumainia vitu vilivyokufa, wale wanaoviita miungu vitu vilivyotengenezwa kwa mikono ya binadamu: Vitu vya dhahabu na fedha vilivyotengenezwa kwa ustadi; sanamu za wanyama, au hata jiwe lisilo na faida, alilochonga mtu wa kale.
11 Mkata miti hukata mti fulani ufaao, kisha huondoa maganda yake, akachonga kwa ustadi chombo kizuri cha kufaa.
12 Huchukua vipande vilivyosalia akajipikia chakula akala shibe yake.
13 Lakini aweza kuokota kipande kimojawapo kisichofaa chochote, kipande kilichopindika na chenye mafundo tele, akakichonga kwa uangalifu wakati wa mapumziko, na kukipa umbo wakati hana cha kufanya, akafaulu kukifanya kuwa mfano wa binadamu
14 au ya mnyama fulani duni. Hukipaka rangi nyekundu na kufunika hitilafu yoyote kwa rangi.
15 Kisha hukitengenezea mahali maalumu ukutani na kukifunga kwa chuma kisianguke,
16 maana anajua dhahiri kwamba ni sanamu tu na inahitaji kusaidiwa; haiwezi kujitegemeza.
17 Wakati wa kuomba dua kuhusu mali yake, harusi au watoto, hana aibu kabisa kukiomba kitu hicho kisicho na uhai!
18 Naam, hukiomba kitu hicho dhaifu afya, hukiomba uhai kitu hicho kisicho na uhai, hukiomba msaada kitu hicho kisicho na maarifa, hukiomba safari njema kitu hicho kisichoweza kwenda hata hatua moja!
19 Naam, anaomba faida, mapato na mafanikio kazini, kwa kitu ambacho mikono yake haina nguvu yoyote!

Generic placeholder image