8

1 Nguvu ya Hekima huenea kila mahali duniani na kuweka kila kitu katika mpango mzuri.

Upendo wa Solomoni kwa Hekima
2 Nilimpenda Hekima na kumtafuta tangu ujana wangu; nilitamani kumchukua awe mchumba wangu, nikavutwa sana na uzuri wake.
3 Hekima hutukuza mwanzo wake maarufu kwa kuishi pamoja na Mungu, naye Bwana mkuu wa yote anampenda.
4 Hekima anafahamu mafumbo ya Mungu na anashiriki matendo yake.
5 Kama mali ni kitu cha kutamanika katika maisha haya, utajiri ni nini ukilinganishwa na Hekima aongozaye mambo yote?
6 Kama maarifa ni kitu cha kufaa kuwa nacho, hakuna kilicho bora kuliko Hekima atengenezaye yote.
7 Je, wapenda uadilifu? Basi, matokeo ya kazi ya Hekima ni adabu njema, kuwa na kiasi, maarifa, haki na ushujaa. Maishani hakuna kilicho bora kupita hayo.
8 Je, wataka kuwa na ujuzi mwingi? Hekima ajua mambo ya kale na hutangulia kujua yajayo; hujua kufafanua mafumbo ya watu na kutatua matatizo. Hujua maana ya ishara na maajabu na huweza kubashiri matokeo ya majira na nyakati.
9 Basi niliamua kumchukua nikae naye, nikijua kwamba atanipa mashauri mema na kunipa moyo wakati wa shida na huzuni.
10 Kwa sababu yake nitaheshimika wanapokutana watu, wazee wataniheshimu ingawa mimi ni kijana.
11 Wataona kwamba uamuzi wangu ni wa busara, nao watawala watanistahi.
12 Nikinyamaa wataningoja niseme, na nikisema watatega masikio. Hata nikisema kwa muda mrefu watanisikiliza kwa makini.
13 Kwa sababu ya Hekima nitajaliwa hali ya kutokufa, nao watakaoishi baada yangu watanikumbuka daima.
14 Nitakuwa na madaraka juu ya watu na mataifa;
15 watawala wa mabavu wataniogopa wakisikia habari zangu. Miongoni mwa watu wangu nitakuwa mwenye uwezo na hodari vitani.
16 Niingiapo nyumbani nitapumzika pamoja naye, maana kukaa pamoja naye hakuna huzuni kushirikiana naye hakuna uchungu bali furaha na shangwe.
17 Ninapoyatafakari mambo haya moyoni mwangu, na kuyafikiria akilini mwangu, kwamba kutokufa kwapatikana kwa kuwa na Hekima,
18 kwamba wanaompenda hupata furaha kamili, wanaofanya kazi zake hupata mali isiyopungua, wanaozungumza naye huwa wenye maarifa, na wanaopatana na maneno yake huongezwa heshima; basi nilizunguka nikitafutatafuta jinsi ya kumchukua huyo Hekima.
19 Nilipokuwa mtoto nilikuwa na vipaji vya kuzaliwa, nilibahatika kuwa na roho njema, 20au tuseme, nilikuwa mwema, nikaingia katika mwili safi.
21 Lakini nilitambua kwamba singeweza kupata Hekima nisipopewa na Mungu; na huko kujua kwamba Mungu aweza kunipa, ni alama ya maarifa. Kwa hiyo nilimwomba Bwana na kumsihi kwa moyo wangu wote nikasema:

Generic placeholder image