15

Mungu wa kweli
1 Lakini wewe, Mungu wetu, ni mwenye wema na kweli, wewe ni mvumilivu na watawala vyote kwa huruma.
2 Hata tukitenda dhambi twajua nguvu yako, nasi tu watu wako. Lakini hatutatenda dhambi kwa kuwa tunajua kwamba sisi ni wako.
3 Maana kukujua wewe ni uadilifu kamili, kutambua nguvu yako ni chanzo cha kuishi milele.
4 Sisi hatukupotoshwa kwa kazi mbaya za ufundi wa binadamu, au kwa kitu duni kilichotiwa nakshi na msanii, kinyago kilichopakwa rangi mbalimbali,
5 ambacho umbo lake huamsha tamaa za watu wajinga na kuwafanya watamani sanamu isiyo na uhai wowote.
6 Wanaotengeneza vitu kama hivyo, na wanaotamani kuviabudu, wote wangangania uovu.
7 Mfinyanzi huukanda udongo laini akafinyanga kila chombo kwa uangalifu kwa matumizi yetu. Hutumia udongo huo huo kufinyangia vyombo: Vingine kwa matumizi safi na vingine kwa matumizi yasiyo safi. Vyombo vyote hivyo huviunda namna moja. Lakini ni vyombo vipi kwa matumizi yapi, mfinyanzi mwenyewe huamua.
8 Tena kwa kazi bure mfinyanzi huunda mungu duni kwa udongo ule ule, hali yake mwenyewe ni kiumbe kifacho kilichoundwa hivi, punde tu na wakati ufikapo wa kurudisha roho yake aliyokopeshwa, atarudi udongoni ambamo alitolewa.
9 Lakini yeye hajali kwamba kifo kinamkabili, wala kwamba maisha yake ni mafupi; ila hushindana na mafundi wa vyombo vya dhahabu na fedha na kuiga mafundi watumiao shaba, na kuona fahari kwa kufinyanga miungu ya kuiga.
10 Moyo wake ni majivu na tumaini lake ni hafifu kuliko vumbi. Uhai wake hauna thamani kama udongo,
11 kwa sababu hajapata kamwe kumtambua Mungu aliyemwumba, Mungu aliyemjalia roho mwenye nguvu ya kutenda, alimpulizia pumzi ya uhai.
12 Mtu huyo hufikiria maisha yetu kuwa mchezo tu, na uhai wetu kuwa tamasha la kujipatia faida. Husema ni lazima kupata fedha kwa vyovyote vile hata kama ni kwa njia isiyofaa.
13 Mtu huyo ambaye kwa udongo ule ule hufinyanga sanamu za miungu na vyombo vivunjikavyo, ajua kuliko wengine wote kwamba anatenda dhambi.
14 Lakini wapumbavu kuliko wote na wanaosumbuka kuliko watoto wachanga, walikuwa wale maadui ambao waliwatesa watu wako.
15 Wao walidhani sanamu za watu wasiomjua Mungu ni miungu, ingawaje hazina macho ya kuona wala pua za kuvuta pumzi, wala masikio ya kusikia, wala vidole vya kupapasa, na miguu yao haifai kitu kwa kutembea.
16 Binadamu ndiye aliyezitengeneza, mtu ambaye roho yake amekopeshwa ndiye aliyezifanya. Hakuna mtu awezaye kutengeneza mungu aliye bora kuliko binadamu.
17 Mtu hufa, lakini hutengeneza kitu ambacho chenyewe kimekufa fofofo. Yeye binafsi ni bora kuliko hicho kitu anachokiabudu. Naam, yeye ana uhai, lakini hicho kitu anachokiabudu hakina uhai kabisa.
18 Watu hao huabudu hata wanyama wa kuchukiza kabisa ambao hata kwa akili ni duni kuliko viumbe vingine vyote.
19 Hata ukivilinganisha na viumbe vingine, hivi havitamaniki kabisa. Vyenyewe havikuwahi kupata sifa na baraka ya Mungu.

Generic placeholder image