11

1 Hekima aliwafanikisha hao watu wakiongozwa na yule nabii mtakatifu.
2 Walisafiri jangwani pasipokaliwa na watu, wakapiga hema zao mahali ambapo hakuna aliyepitia kabla.
3 Waliwakabili maadui zao na kuwashinda wapinzani wao.
4 Walipoona kiu walikulilia, nawe ukawapa maji kutoka kwenye mwamba mgumu, wakakata kiu yao.
5 Pigo ulilowapa maadui zao liliwasalimisha watu wako taabuni.
6 Badala ya maji ya mto unaotiririka daima, mto uliofurika na kutiwa unajisi kwa damu
7 kama adhabu kwao walioamuru watoto wachanga wauawe wewe uliwapatia watu wako maji mengi ghafla,
8 ukaonesha kwa kiu yao wakati ule, jinsi ulivyowaadhibu maadui zao.
9 Walipojaribiwa, ingawa walikuwa wanapewa nidhamu kwa huruma, walijifunza jinsi waovu walivyoteswa wakati ulipowahukumu kwa hasira.
10 Uliwaonya kama vile baba aonyavyo watoto wake. Lakini uliwachunguza hao waovu kama mfalme mkali anapohukumu.
11 Wakiwa mbali au wakiwa karibu wote waliteseka,
12 Walipata majonzi maradufu kwa kukumbuka yaliyotukia.
13 Waliposikia kwamba adhabu yao iliwafaidia watu wako, walikiri kwamba wewe, ee Bwana, ndiwe uliyeyatenda hayo.
14 Ingawa walikuwa wamemdharau yule ambaye hapo awali alikuwa ametupwa na kuachwa, baada ya matukio hayo yote walimstaajabia, waliposikia kiu kali kuliko ya watu waadilifu.
15 Kwa sababu ya upumbavu na mawazo yao maovu ambayo yaliwapotosha wakaabudu nyoka na wanyama duni, wewe uliwaleta viumbe wasio na akili wawaadhibu,
16 wajifunze kwamba mtu huadhibiwa kwa vitu vilevile alivyotenda navyo dhambi.
17 Kwa mkono wako wenye nguvu zote ambao uliumba ulimwengu bila kutumia chochote chenye umbo, umekuwa daima wenye uwezo na ungaliweza kwa urahisi kuwaletea dubu wengi au simba wakali,
18 au wanyama wakali sana ambao hawajapata kuwako, au wanyama watoao pumzi ya moto au wanaopumua moshi mzito wenye kudhuru, au watoao machoni mwao cheche za kutisha.
19 Sio tu kwamba mashambulio ya hao wanyama yangeua watu ila kule tu kuwaona watu wangekufa kwa kutishwa.
20 Licha ya hao, ungaliweza kuwaangamiza kwa pumzi moja tu wakifuatiwa na haki yako, au kuwatawanya kila mahali kwa mvumo wa uwezo wako. Lakini wewe umepanga kufanya kila kitu kwa kipimo, taratibu na uzito.

Mungu ni mwenye nguvu na huruma
21 Kuwa na uwezo mkuu ni hadhi yako daima, na hakuna mtu awezaye kuikabili nguvu ya mkono wako.
22 Kwako, ulimwengu wote ni kama chembe moja katika mizani; ni kama tone moja la umande wa asubuhi juu ya ardhi.
23 Lakini wewe ni mwenye huruma kwa wote maana waweza yote; waacha kuzijali dhambi zetu ili tupate kutubu.
24 Wewe wapenda vitu vyote vilivyopo, wala huchukii chochote ulichokiumba. Hungaliumba chochote kile kama ungekuwa unakichukia.
25 Chawezaje chochote kudumu ila kwa kupenda kwako? Chawezaje kuendelea kuwako kama hungalikiumba?
26 Umeruhusu vitu vyote viwepo ee Bwana, kwa maana ni vyako, nawe wapenda vitu vyote hai.

Generic placeholder image