7

Mfalme ni sawa na watu wengine
1 Mimi ni binadamu ambaye hufa, sawa na wengine, mzawa wa yule mtu wa kwanza aliyeumbwa kutoka kwa udongo. Nilitengenezwa nikawa mwili tumboni mwa mama yangu
2 kwa muda upatao miezi tisa, baada ya kuwekwa pamoja kwa mbegu ya mtu na kwa furaha ya ndoa.
3 Nami nilipozaliwa, nilianza kupumua hewa ya kawaida nilitua juu ya ardhi yenye asili moja nami, na sauti ya kwanza niliyotoa ilikuwa kilio kama wengine.
4 Nilivikwa nguo za kitoto, nikatunzwa kwa uangalifu.
5 Hakuna mfalme yeyote aliyeanza kuishi kwa namna nyingine;
6 maana wote huingia duniani kwa njia moja na hutoka humo kwa njia moja.

Solomoni anathamini Hekima
7 Basi, niliomba, nami nikapewa maarifa; nilimwomba Mungu, nayo roho ya Hekima ikanijia.
8 Nilimthamini Hekima kuliko viti vya enzi na mamlaka, nikaona utajiri si kitu ukilinganishwa naye.
9 Sikumfananisha na johari yenye thamani kubwa, maana dhahabu yote duniani ni kama mchanga, na fedha ni kama udongo tu mbele yake.
10 Nilimpenda Hekima kuliko afya na urembo, nilimpendelea kuliko mwanga wa jua, maana mwangaza wake haufifii kamwe.
11 Mema yote yalinijia pamoja na Hekima; mikononi mwake nilipata mali isiyohesabika.
12 Niliyafurahia hayo yote maana aliniletea Hekima; lakini sikujua kwamba Hekima ndiye mama wa hayo yote.
13 Nilijifunza bila hila na kufunza bila lalamiko; utajiri wake sikuwaficha watu.
14 Hekima ni hazina isiyomalizika kwa watu; wanaopata Hekima hujipatia urafiki na Mungu; yeye huthibitisha yote wanayojifunza kutoka kwake.
15 Namwomba Mungu anijalie kunena kadiri atakavyo, na mawazo yangu yastahili yale niliyojifunza. Mungu mwenyewe ndiye kiongozi wa Hekima; yeye huwakosoa wale walio na busara.
16 Sisi tumo mikononi mwake, pamoja na maneno yetu; naam, sisi, maarifa yetu na ufundi wetu.
17 Yeye ndiye aliyenijalia ujuzi sahihi wa nguvu za maumbile: Ulimwengu ulitengenezwa kwa kitu gani, na maunganisho ya maumbile yake,
18 mianzo ya nyakati, miisho yake na katikati yake, zamu za vituo vya jua na mabadiliko ya majira,
19 mfululizo wa miaka, na makundi ya nyota.
20 Amenifundisha juu ya asili ya viumbe hai, hisia za wanyama wa porini, nguvu za roho, uwezo wa akili ya binadamu, mimea mbalimbali na matumizi ya mizizi yake.
21 Nilijifunza mambo yaliyofichika na yaliyo dhahiri, maana Hekima, mratibu wa mambo yote, alinifundisha.

Maumbile Yya Hekima
22 Katika Hekima kuna roho ya maarifa na utakatifu; roho ya pekee inayojidhihirisha kwa namna nyingi, nyepesi sana na yenye kumudu kwa urahisi; dhahiri, safi, wazi, na isiyoweza kuharibiwa; yenye kupenda wema, hodari na isiyoshindwa na chochote;
23 yenye ukarimu na yenye kupenda watu; roho thabiti, yenye kuaminika na isiyo na wasiwasi; yenye nguvu na uwezo wa kuona yote; yenye kupenya kila chenye akili, kilicho safi na chenye werevu wa hali ya juu.
24 Hekima huenda kwa urahisi kuliko mwendo wowote; ni safi hivyo kwamba hupenya na kuenea ndani ya kila kitu.
25 Hekima ni pumzi ya nguvu ya Mungu, mmiminiko safi wa utukufu wa Mungu Mwenye Nguvu; hivyo, chochote kilicho najisi hakiwezi kumwingia.
26 Hekima ni mngao wa mwanga wa milele, kioo safi cha matendo ya Mungu na mfano wa wema wake.
27 Ingawa Hekima ni mmoja aweza kutenda chochote, habadiliki, ingawa hufanya upya kila kitu. Katika vizazi vyote huingia rohoni mwa watu watakatifu na kuwafanya marafiki wa Mungu na manabii.
28 Maana Mungu humpenda tu mtu akaaye na Hekima.
29 Hekima ni mzuri kuliko jua na apita makundi yote ya nyota; ni bora kuliko mwanga wa mchana,
30 maana baada ya mchana huja usiku, lakini uovu hauwezi kumshinda Hekima.

Generic placeholder image