18

Mwanga wawaangazia watu wa Israeli
1 Lakini, mwanga mkubwa uliwaangazia watu wako watakatifu. Maadui zao walisikia sauti zao lakini hawakuweza kuwaona; waliona watu wako wana bahati kwa vile hawakuteseka.
2 Hao maadui angalau walishukuru kwamba watu wale ambao waliwatesa hapo awali hawakuwalipiza kisasi, na hivyo wakawasihi wajiendee zao.
3 Kisha ukawapatia watu wako mnara wa mwanga wa moto uwaongoze katika njia ambayo hawakuijua, mwangaza mtulivu katika safari hiyo tukufu.
4 Lakini maadui zao wakanyimwa mwanga huo, wakastahili kufungwa gizani hao waliokuwa wamewafunga watu wako, ambao kwa njia yao ulimwengu ungepewa mwanga wa milele wa sheria yako.

Kifo cha wazaliwa wa kwanza wa Misri
5 Wakati maadui hao walipoamua kuwaua watoto wachanga wa watu wako, na yule mtoto mchanga alipoachwa na kuokolewa baadaye, wewe uliwaadhibu kwa kuua idadi kubwa ya watoto wao, na kuwaangamiza wote katika mafuriko makubwa.
6 Lakini wazee wetu walijulishwa juu ya usiku huo ili wakiwa wanajua wapate moyo na kufurahia ahadi walizopewa.
7 Watu wako walitazamia kuokolewa kwa waadilifu na kuangamizwa kwa maadui zao.
8 Kwa kitendo hichohicho cha kuwaadhibu maadui zetu ulitujalia heshima tukufu ya kutuita kwako.
9 Kwa siri, watu hao wema wa taifa adilifu walitolea tambiko na kwa moyo mmoja wakatekeleza sheria ya Mungu watu watakatifu washiriki pamoja: Baraka na hatari, wakawa tayari wanaimba sifa za wazee wao.
10 Lakini sauti za maadui zao zilisikika kila mahali wakiomboleza vifo vya watoto wao.
11 Watumwa walipata adhabu ileile waliyopata mabwana zao; watu wa kawaida wakapata hasara sawasawa na mfalme.
12 Wote pamoja walikufa kwa njia ileile; maiti zilikuwa nyingi mno na waliobaki hai hawakutosha kuzizika. Kwa pigo moja tu, watoto wao waliowapenda mno walikufa.
13 Watu hao hawakujali onyo lolote ila walitegemea uchawi wao. Lakini watoto wao wa kwanza walipoangamizwa, walitambua kwamba watu hao walikuwa watoto wa Mungu.
14 Kulipokuwa shwari kabisa, kila mahali, na usiku ukiwa umefikia nusu ya safari yake,
15 Neno wako wa nguvu kuu akashuka kutoka mbinguni, naam, kutoka kwenye kiti chako cha enzi, akiwa kama mtu shujaa wa vita, aliishukia nchi iliyohukumiwa kuangamizwa,
16 ameshika upanga mkali wa kutekeleza amri yako thabiti. Alisimama na vitu vyote vikakumbwa na kifo, aligusa mbingu kwa kichwa chake akiwa amesimama juu ya nchi.
17 Mara, watu wale wakapatwa na maono ya kutisha na ndoto za kuogopesha zikawavamia.
18 Walilala kila mahali nchini wamezirai huku wakionesha sababu ya kifo chao.
19 Ndoto zao za kutisha ziliwadhihirishia jambo hilo, ili wasije wakafa kabla ya kujua sababu ya mateso yao.

Ombi la Aroni lawaokoa watu wa Israeli katika kifo
20 Waadilifu pia iliwabidi kuonja kifo; ugonjwa mbaya uliwavamia wengi kule jangwani, lakini hasira yako haikudumu muda mrefu.
21 Mtu mmoja asiye na hatia aliharakisha kuwaombea. Yeye, kama vile kasisi, alifanya maombi na kufukiza ubani wa upatanisho, na hivyo akaonesha kwamba alikuwa mtumishi wako. Hizo zikiwa silaha zake, aliikabili hasira yako na kuyakomesha yale maafa.
22 Aliyashinda yale maafa si kwa nguvu za kibinadamu wala kwa silaha za vita, ila kwa sala aliikomesha ile adhabu akikumbusha ahadi na maagano uliyowapa wazee wetu.
23 Maiti zilipokuwa zimerundikana, yeye aliingilia kati na akaikinga hasira yako, akaizuia isiwapate wale waliokuwa bado hai.
24 Alikuwa amevaa vazi refu lililochorwa alama za ulimwengu, na kifuani alivaa sifa za wazee wetu zimechorwa katika safu nne za vito, na kichwani kilemba kilichopambwa kuonesha enzi yako.
25 Mharibifu aliyaogopa hayo, akakata tamaa. Uliwaonjesha tu hasira yako lakini hiyo ilitosha.

Generic placeholder image