5


1 Siku hiyo, mtu mwema atasimama kwa ujasiri mwingi, mbele yao hao waliokuwa wanamtesa na wale ambao walipuuza kazi zake.
2 Watakapomwona watatetemeka kwa hofu kubwa, watashangaa ameokolewaje bila wao kutazamia.
3 Ndipo watakapojuta na kusemezana wao kwa wao na kwa kuugua moyoni wataambiana:
4 “Huyu ndiye mtu yuleyule tuliyemdhihaki zamani, tukamwona ni kichekesho; kweli tulikuwa wapumbavu. Tulidhani aliishi kama mwendawazimu, na alipokufa hatukumpa heshima.
5 Imekuwaje sasa yuko pamoja na watoto wa Mungu na anayo sehemu yake kati ya watakatifu wake!
6 Kumbe sisi ndio tuliokiuka njia ya kweli! Hatukuishi katika mwanga wa haki, wala mwanga wake haukutuangaza.
7 Sisi tulijaa upotovu na uharibifu; tulitangatanga jangwani pasipo njia, wala hatukujua njia ya Bwana.
8 Kujigamba kwetu kumetufaa nini? Tumepata faida gani kwa utajiri tuliojivunia?
9 Vitu hivyo vyote vimepita kama kivuli; naam, kama minongono inayotoweka.
10 Ni kama meli ipasuayo mawimbi baharini, lakini ikisha pita alama yake haionekani, wala mkondo wake katika mawimbi.
11 Au kama vile ndege arukavyo angani: Haachi alama yoyote ya njia yake; huipigapiga hewa nyepesi kwa mabawa yake, huipenya kwa nguvu za kuruka kwake, na huipasua kwa mapigo ya mabawa yake, lakini haachi alama yoyote ya kupita kwake.
12 Kadhalika mshale: Unapofyatuliwa kulenga shabaha, hupenya hewa, lakini hewa hufumba mara moja; wala hakuna mtu awezaye kutambua ulipopitia.
13 Kadhalika nasi, mara baada ya kuzaliwa twatoweka, bila hata kuacha nyuma alama yoyote ya wema, bali tuliangamia katika uovu wetu wenyewe.”
14 Matumaini ya mwovu ni kama makapi yapeperushwayo na upepo; ni kama povu linalochukuliwa na tufani; hutawanywa kama moshi mbele ya upepo, hupita kama kumbukumbu ya mgeni wa siku moja.
15 Lakini watu wema huishi milele na tuzo lao liko kwa Bwana; naam, Mungu Mkuu huwatunza.
16 Kwa hiyo watapokea taji tukufu, na kilemba maridadi mkononi mwa Bwana, maana kwa mkono wake wa kulia atawafunika, kwa mkono wake atawakinga kama kwa ngao.
17 Atautwaa upendo wake mkuu kama zana za vita; atavipa silaha viumbe vyote kufukuza maadui zake.
18 Haki itakuwa kama vazi la kujikinga kifua, hukumu ya haki itakuwa kama kofia yake ya chuma;
19 utakatifu utakuwa ndio ngao yake imara.
20 Atainoa ghadhabu yake kali kuwa upanga, na ulimwengu wote utajiunga naye kupigana na maadui wasio na akili.
21 Umeme utaruka moja kwa moja na kupiga shabaha, kama mishale kutoka uta imara mawinguni.
22 Mvua ya mawe itawalenga kama kwa uta na mshale; maji ya bahari yatafurika kwa hasira dhidi yao, na mito itawaangamiza bila huruma.
23 Upepo mkali utazuka dhidi yao, na kuwapeperushia mbali kama kimbunga. Upotovu utasababisha maangamizi nchini kote; matendo maovu yataporomosha mamlaka ya watawala.

Generic placeholder image