6

Jukumu la watawala
1 Sikilizeni basi, enyi wafalme, mkaelewe; jifunzeni, enyi waamuzi popote duniani.
2 Tegeni sikio nyinyi mnaotawala watu wengi, na kujisifia wingi wa mataifa.
3 Mamlaka hayo mlipewa na Bwana; na utawala mliupata kwa Mungu Mkuu. Atazipima kazi zenu na kuchunguza mipango yenu.
4 Maana, kama watumishi katika utawala wake, hamtawali kwa uadilifu, kama hamshiki sheria, wala kufuata mwongozo wa Mungu,
5 yeye atawajia ghafla na kuwapeni adhabu kali, maana adhabu kali huwapata aghalabu wenye madaraka.
6 Watu wa kawaida wanaweza kusamehewa kutokana na huruma; lakini wenye madaraka watakabiliwa na uchunguzi mkali.
7 Maana Bwana wa wote hamwogopi mtu yeyote, ukuu wa mtu hauwezi kumfanya apendelee; Yeye mwenyewe aliwafanya wote, wakubwa na wadogo na huangalia mahitaji ya wote kwa usawa.
8 Lakini wenye madaraka watakabiliwa na uchunguzi mkali.
9 Basi, maneno yangu yawahusu nyinyi wafalme, ili mjifunze kuwa na hekima, msije mkakosa.
10 Maana wanaozingatia mambo matakatifu watakubaliwa kuwa watakatifu. Waliofunzwa hayo watapata humo cha kujitetea hukumuni.
11 Basi, muwe na hamu ya mafundisho yangu; yatamani yawaongoze nanyi mtapata nidhamu.

Thamani ya Hekima
12 Hekima huangaza wala hafifii. Wanaompenda Hekima humwona kwa urahisi, wanaomtafuta Hekima humpata.
13 Hekima hutangulia kujionesha kwa wale wanaomtaka.
14 Ukiamka mapema asubuhi kumtafuta, hutataabika; utamkuta anakungojea mlangoni pake.
15 Kumsikiliza Hekima kwa makini ni kupata maarifa kamili. Ukimtafuta usiku na mchana hutapata masumbuko.
16 Hekima daima huwatafuta wale wanaomstahili; njiani hujidhihirisha kwao kwa upendo, yu pamoja nao katika kila wazo.
17 Mwanzo wa Hekima ni hamu kubwa ya kufunzwa; kujali mafundisho ni kumpenda Hekima,
18 kumpenda ni kushika sheria zake; kushika sheria zake ni uhakika wa kutokufa.
19 na kutokufa kwamleta mtu karibu na Mungu.
20 Hivyo hamu ya kumpata Hekima huongoza kwenye ufalme.
21 Basi, enyi watawala wa watu, kama mwafurahia viti vyenu vya enzi na alama za mamlaka juu ya watu, mheshimuni Hekima mpate kutawala milele.

Nia ya kuwashirikisha wengine Hekima
22 Nitawaambieni Hekima ni nani na chanzo chake. Sitawaficheni siri yoyote ile; nitawaambieni historia yake yote tangu mwanzo wake, na kudhihirisha wazi habari zake bila kuacha ukweli wowote ule.
23 Wivu ule mbaya kamwe hautakuwa mwenzangu, maana Hekima hapatani na hali ya wivu.
24 Wingi wa wenye Hekima ni wokovu kwa ulimwengu, mfalme mwenye busara ni uthabiti wa watu wake.
25 Kwa hiyo basi, mfunzwe na maneno yangu, nanyi mtapata faida.

Generic placeholder image