12

Malaika Rafaeli
1 Baada ya sherehe za harusi, Tobiti alimwita mwanawe Tobia, akamwambia, “Mwanangu, hakikisha kwamba unamlipa rafiki yako aliyesafiri nawe mshahara wake na kumwongezea kitu.”
2 Tobia akamwuliza, “Baba, nitamlipa kiasi gani? Hata kama nikimpa nusu ya mali tuliyoleta pamoja singejali.
3 Yeye amenifikisha nyumbani salama salimini; alimponya mke wangu, akaileta ile fedha pamoja nami, na sasa amekuponya wewe! Nitampa nini kwa hayo yote?”
4 Tobiti akajibu, “Anastahili nusu ya yote aliyokusaidia kupata.”
5 Basi, Tobia akamwita Rafaeli, akamwambia, “Chukua nusu ya mali yote uliyonisaidia kupata, kama mshahara wako. Nakutakia safari njema!”
6 Lakini Rafaeli akawaita faraghani Tobiti na Tobia, akawaambia, “Mtukuzeni Mungu; tangazeni sifa zake kwa watu wote kwa ajili ya fadhili alizowafanyia. Mtukuzeni na kulisifu jina lake. Watangazieni watu wote matendo ya Mungu kama ipasavyo na wala msichoke kumshukuru.
7 Yafaa kutunza siri ya mfalme, lakini matendo ya Mungu ni lazima yatangazwe kila mahali kama ipasavyo. Tendeni mema nanyi hamtapata madhara.
8 “Afadhali sala pamoja na ukweli na kusaidia maskini pamoja na kutenda haki kuliko kuwa tajiri na kukosa uaminifu. Afadhali kusaidia maskini kuliko kulimbikiza dhahabu.
9 Sadaka kwa maskini humwokoa mtu na kifo na kumtakasa dhambi zake zote. Wale wanaowasaidia maskini watajaliwa uhai,
10 lakini wale wanaotenda dhambi na kufanya uovu hujiletea madhara wao wenyewe.
11 “Sasa nitawajulisheni ukweli wote bila kuwaficheni chochote. Nilikwisha waambia kwamba yafaa kuitunza siri ya mfalme, lakini matendo ya Mungu lazima yatangazwe kila mahali kama ipasavyo. Tobiti!
12 Wewe na Sara mlipokuwa mnasali wakati ule, mimi ndiye niliyewasilisha sala zenu mbele ya Bwana aliye mtukufu. Na kila ulipokuwa unawazika wafu, mimi niliwasilisha matendo yako mbele yake.
13 Wakati wewe hukusita hata kidogo kuinuka na kukiacha chakula ukaenda kumzika mtu aliyekufa, Mungu alinituma nikujaribu.
14 Lakini pia alinituma kukuponya na kumwokoa mke wa mwanao, Sara.
15 Mimi ni Rafaeli, mmoja wa wale malaika saba wanaokaa tayari daima mbele yake Bwana aliye mtukufu kumtumikia.”
16 Tobiti na Tobia wakashikwa na hofu kubwa, wakasujudu wakiogopa sana.
17 Lakini Rafaeli akawaambia, “Msiogope! Muwe na amani. Mtukuzeni Mungu milele.
18 Mimi nilipokuwa kati yenu haikuwa kwa kutaka kwangu mwenyewe, bali kwa kutaka kwake Mungu. Yeye ndiye mnayepaswa kumtukuza maisha yenu yote. Yeye ndiye mnayepaswa kumsifu.
19 Nyinyi mlidhani mliniona nikila chakula, lakini ni kwa kuonekana tu na haikuwa hivyo.
20 Basi, sasa mtukuzeni Bwana duniani na kumshukuru. Mimi narudi sasa kwake yeye aliyenituma kutoka juu. Andikeni mambo hayo yote yaliyotukia.”
21 Kisha Rafaeli akatoweka, wasimwone tena. 22Basi wakamsifu Mungu kwa nyimbo, wakamshukuru kwa ajili ya matendo yake makuu aliyowafanyia malaika wake Mungu alipokuwa amewatokea.

Generic placeholder image