3

Sala ya Tobiti
1 Basi mimi kwa uchungu mkubwa nilianza kusononeka na kutoa machozi, kisha nikaanza kusali kwa huzuni:
2 “Ee Bwana, wewe ni mwenye haki, matendo yako yote ni ya haki; hatua zako ni za rehema na ukweli Wewe ndiwe unayeuhukumu ulimwengu.
3 Basi ee Bwana unikumbuke na kuniangalia; usiniadhibu kwa sababu ya dhambi zangu, wala kwa sababu ya makosa yangu, au makosa waliyofanya wazee wangu.
4 Wao hawakuzitii amri zako; kwa hiyo ukatuacha tushambuliwe, tuhamishwe na kuuawa. Ulitufanya kuwa fedheha na dharau miongoni mwa mataifa yote tulimotawanywa.
5 Mara nyingi umewahukumu babu zangu kadiri ya dhambi zao na mimi umeniadhibu kadiri ya dhambi zangu. Tulikosa uaminifu, tukavunja amri zako, kwa hiyo daima tuliadhibiwa kwa haki.
6 Sasa unifanye utakavyo. Uitoe roho yangu, nitoweke hapa duniani, mwili wangu na uwe tena udongo. Kwangu afadhali kufa kuliko kuishi, maana nashutumiwa bila makosa; nimekata tamaa kabisa. Bwana, upende basi kuniondoa kwenye msiba huu, unipeleke kwenye pumziko la milele. Usinikatalie ombi langu.”

Matatizo ya Sara
7 Siku hiyohiyo, katika mji wa Ekbatana huko Media, Sara binti Ragueli, naye alitukanwa na mmoja wa watumishi wa kike wa baba yake.
8 Huyu Sara alikuwa ameolewa mara saba, lakini jini Asmodeo lilimuua kila mume kabla mume huyo hajalala na Sara. Basi, huyo mtumishi wa kike akamwambia Sara, “Ewe mwuaji wa wanaume! Ona aibu! Umekwisha kuwa na wanaume saba, lakini hata mmoja wao hakukupatia mwana.
9 Kwa nini watunyanyasa sisi? Nenda zako, uwafuate wanaume zako marehemu. Heri tusione hata mtoto aliyezaliwa na wewe!”
10 Sara aliposikia maneno hayo alihuzunika sana na kutoa machozi, akapanda ghorofani akitaka kujinyonga. Lakini alipotafakari, akasema, “La! Sitajinyonga! Watu wasije wakamdharau baba yangu na kusema, ‘Ulikuwa na mtoto mmoja tu, binti ambaye ulimpenda sana, lakini alijinyonga kwa sababu ya uchungu!’ Jambo kama hilo litasababisha kifo cha baba yangu mzee, nami nitakuwa na hatia. Sitajiua mwenyewe, hasha; nitamwomba Bwana achukue roho yangu, nisisikie tena matusi kama yale!”

Maombi ya Sara
11 Kisha Sara alisimama dirishani, akainua mikono yake na kusali: “Utukuzwe, ee Bwana Mungu wangu; liheshimiwe milele jina lako takatifu.
12 Na sasa, ee Bwana, nimeelekeza macho yangu kwako, nikitumaini utanisaidia.
13 Amuru niondolewe duniani ili nisisikie tena mashutumu.
14 Wajua, ee Bwana, kwamba ningali bikira, sijaguswa na mwanamume.
15 Sijalichafua jina langu wala jina la baba yangu nchini humu nilikohamishiwa. Mimi ni mtoto wa pekee wa baba yangu, yeye hana mtoto mwingine wa kumrithi, wala hana jamaa ambaye ataweza kunioa. Nimekwisha poteza wanaume saba; kwa nini niendelee kuishi? Kama hupendi kuniondoa duniani, walau uniangalie kwa huruma. Siwezi kustahimili kuendelea kushutumiwa!”

Mungu asikiliza sala za Tobiti na Sara
16 Basi, maombi ya Tobiti na Sara yakakubalika mbele yake Mungu mwenyewe, 17naye akamtuma malaika Rafaeli kuwasaidia. Alitumwa kuondoa vile vigamba vyeupe machoni mwa Tobiti ili aweze kuona tena, na kufanya mipango ya ndoa kati ya Sara na Tobia, mwana wa Tobiti; Tobia alikuwa binamu ya Sara, na hivi alikuwa na haki ya kumwoa Sara. Rafaeli aliagizwa pia kuliondoa lile jini Asmodeo, lililokuwa limempagaa Sara. Naam, dakika ileile Tobiti alipoingia nyumbani mwake kutoka uani, Sara naye alikuwa akishuka kutoka ghorofani.

Generic placeholder image