8

Jini latimuliwa
1 Baada ya kula, wazazi wa Sara walimwongoza kijana Tobia chumbani kwa bibiarusi.
2 Tobia alikumbuka maagizo ya Rafaeli. Basi, akafungua mfuko wake, akatoa ini na moyo wa samaki, akaviweka juu ya moto wa ubani; moshi ukafuka.
3 Harufu yake ikalitimulia mbali lile jini, likakimbilia Misri. Rafaeli akalifuatia huko na bila kukawia akalikaba na kulifunga.

Sala ya Tobia
4 Basi Tobia na Sara walibaki peke yao chumbani baada ya wale wazazi kwenda zao na milango kufungwa. Kisha Tobia aliondoka kitandani, akamwambia mkewe, “Inuka, dada, tumwombe Bwana atuonee huruma na kutukinga salama.”
5 Sara akainuka. Tobia akaanza kusali: “Utukuzwe ee Mungu wa wazee wetu. Jina lako lisifiwe milele na milele. Mbingu zikutukuze, navyo viumbe vyako vyote, milele na milele.
6 Ndiwe uliyemuumba Adamu; ndiwe uliyemuumba Hawa mkewe, amsaidie na kumtegemeza. Binadamu wote wametokana na hao wawili. Ndiwe uliyesema: Si vizuri mwanamume kuwa peke yake; Tumuumbe mtu wa kumsaidia aliye kama yeye.
7 Kwa hiyo namchukua dada yangu si kwa sababu ya tamaa ya mwili ila nafanya hivyo kwa dhamiri safi. Uwe na huruma kwake na kwangu utufikishe uzeeni pamoja!”
8 Wote wawili wakaitikia, “Amina! Amina.”
9 Kisha wakalala usiku huo. Wasiwasi wa wazazi Wote walipokuwa usingizini, Ragueli akaamka, akawaita watumishi wake, akaenda nao kuchimba kaburi,
10 maana aliwaza, “Labda na huyo atakufa, na watu watatucheka na kutudhihaki!”
11 Walipomaliza kuchimba kaburi, Ragueli akaingia nyumbani na kumwambia mkewe,
12 “Umtume mtumishi mmoja wa kike akapeleleze kama Tobia angali hai. Kama amekufa, basi, tumzike kabla watu hawajagundua.”
13 Basi, huyo mtumishi alichukua taa, akafungua mlango wa kuingia chumbani kwao. Aliwakuta wote wawili wamelala fofofo.
14 Basi, akarudi na kuwaarifu Ragueli na Edna kwamba Tobia alikuwa bado hai.
15 Hapo Ragueli akamtukuza Mungu wa mbinguni kwa maneno haya:

Sala ya Ragueli “Utukuzwe ewe Mungu wangu kwa sifa za mioyo safi! Utukuzwe milele na milele.
16 Utukuzwe kwa sababu umenifurahisha. Lile nililohofia halikutukia; badala yake umetuonesha huruma yako kuu.
17 Utukuzwe kwa sababu umewarehemu vijana hao wawili watoto wa pekee kwa wazazi wao. Uwajalie ee Bwana huruma na kinga yako; uwajalie maisha ya upendo na furaha.”
18 Halafu Ragueli akaamuru watumishi wake wafukie lile kaburi kabla jua halijachomoza.

Harusi
19 Kisha Ragueli akamwambia mkewe aoke mikate, naye mwenyewe akaenda akachagua ng'ombe wawili na kondoo wanne kutoka kundi la mifugo yake akampata mtumishi atayarishe karamu.
20 Ragueli alimwita Tobia, akamwambia, “Sipendi kusikia juu ya safari yako mpaka baada ya majuma mawili. Utakaa papa hapa ule na kunywa pamoja nami, umfurahishe binti yangu baada ya taabu zote alizopata.
21 Baada ya hapo, utachukua nusu ya mali yangu na kumchukua Sara salama mpaka kwa wazazi wako. Mimi na Edna tutakapofariki utapata ile nusu ya mali yangu iliyobaki. Jipe moyo mwanangu! Tangu sasa mimi ni baba yako na Edna ni mama yako. Tutakuwa wazazi wako hata baadaye kama tulivyo wazazi wa Sara. Jipe moyo mwanangu!”

Generic placeholder image