4

Mawaidha ya Tobiti kwa Tobia
1 Siku hiyohiyo Tobiti akaikumbuka fedha yake aliyokuwa amemwachia Gabaeli kule Rage, nchini Media.
2 Basi akafikiri: “Kwa vile nimemwomba Mungu nife, yanipasa nimwite mwanangu Tobia na kumweleza kuhusu fedha hiyo kabla sijafa.”
3 Basi, Tobiti akamwita Tobia, akamwambia, “Mwanangu, nitakapofariki, unizike ipasavyo. Kisha lazima umheshimu mama yako, umtunze vizuri maisha yako yote. Timiza mambo yote anayotaka uyafanye wala usimhuzunishe kwa vyovyote vile. 4Kumbuka mwanangu jinsi mama yako alivyohatarisha maisha yake apate kukuleta duniani. Basi wakati atakapofariki ni lazima umzike kando yangu katika kaburi moja.
5 “Mwanangu, uwe mwaminifu kwa Bwana Mungu wetu siku zote za maisha yako. Usitende dhambi kwa kusudi, wala usivunje amri zake. Tenda yaliyo mema maisha yako yote wala usifuate njia ya uovu.
6 Maana ukitenda vitu kwa uaminifu utafanikiwa katika mambo yako yote.
7 “Toa sehemu ya mali yako kuwapa maskini. Kamwe usimpe kisogo mtu maskini naye Mungu hatakupa kisogo.
8 Toa ulicho nacho. Ukiwa na zaidi, toa zaidi. Hata kama unacho kidogo tu, toa sehemu yake.
9 Kwa kufanya hivyo utajiwekea hazina bora kwa wakati wa shida.
10 Kwa maana kusaidia maskini huokoa mtu kifoni na kumkinga asiingie katika makao ya giza.
11 Naam! Kusaidia maskini, kwa wale wanaofanya hivyo, ni sadaka bora mbele ya Mungu Mkuu.
12 “Mwanangu, ujihadhari na maisha ya uasherati. Zaidi ya hayo, oa mke kutoka kabila la wazee wako. Usijichagulie mwanamke kuwa mkeo kutoka kabila lisilo la wazee wako kwa kuwa sisi ni wa ukoo wa manabii. Kumbuka kwamba wazee wetu wote, akina Noa, Abrahamu, Isaka na Yakobo, tangu mwanzo walioa wake kutoka koo zao, naye Mungu akawajalia watoto, na hao wazawa wao wataimiliki nchi ya Israeli.
13 Hali kadhalika nawe mwanangu, ni lazima uwapende jamaa zako. Usiwe na majivuno hata ukaacha kuoa kutoka jamaa yako. Majivuno kama hayo huleta maangamizi na hasara kubwa, kama vile uvivu uletavyo ufukara na njaa kali. Maana uvivu ni mama wa njaa.
14 “Usiiweke mishahara ya vibarua wako mpaka kesho yake. Lazima uwalipe mara moja. Kama ukimheshimu Mungu, yeye atakupa tuzo lako. Uwe mwangalifu katika matendo yako yote; uwe na nidhamu katika mwenendo wako.
15 Usimtendee mtu usichotaka kutendewa wewe mwenyewe. “Usinywe pombe na kulewa; ulevi usiwe mwenzio.
16 “Uwapatie chakula wenye njaa, na nguo watu walio uchi. Toa kusaidia maskini kadiri ya wingi wa mali yako, tena unapomsaidia maskini fanya hivyo kwa moyo radhi!
17 Mcha Mungu akifariki, toa chakula kwa ajili ya jamaa yake, lakini usifanye hivyo akifa mtu mwovu.
18 Omba shauri kwa watu wenye busara, wala usidharau shauri lenye kufaa.
19 Umtukuze Bwana Mungu wako siku zote. Umwombe aongoze njia zako na kuzifanikisha shughuli zako. Maana hekima si mali ya kila taifa. Mungu mwenyewe ndiye awapaye mema yote. Akitaka humwangusha mtu hata mpaka kuzimu. Basi Mwanangu uyakumbuke mawaidha yangu wala usiyaache yafutike moyoni mwako.
20 Na sasa mwanangu, napenda kukujulisha kuwa zamani nilimkabidhi fedha nyingi Gabaeli, mwana wa Gabria, huko Rage katika nchi ya Media.
21 Basi, usiwe na hofu kwamba sisi tumekuwa maskini. Kama ukimcha Mungu, ukaepukana na kila dhambi na kutenda yanayompendeza utakuwa na mali nyingi.”

Generic placeholder image